PROF. MKEDA: MFUKO WA UBUNIFU WA SAMIA KUCHOCHEA BUNIFU MPYA
Dar es salaam - Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema Mfuko wa Ubunifu wa Samia, umelenga kuwezesha wabunifu kubiasharisha bunifu zao badala ya kuendelea kushiriki kwenye maonesho.
Amesema sababu ya kuanzishwa kwa mfuko huo ni benki kushindwa kukopesha wabunifu kwa madai kwamba hawakopesheki na kwamba ni bunifu zinazoanza ziko katika hatari.
Ameyasema hayo leo Dar es Salaam wakati akifunga kongamano la tisa la sayansi, teknolojia na ubunifu lililoandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
”Mfuko wa Ubunifu una zaidi ya Sh bilioni 6 ni mtaji kwa wabunifu waweze kuuza bunifu zao. Tunataka bunifu mpya na sio zilezile kila mwaka,” ameeleza Profesa Mkenda.
Pia amesema mfuko huo ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuna fedha kwa watafiti, wabunifu na wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi, teknolojia na ubunifu.
Amesema serikali imetenga fedha kwa ajili ya utafiti wa mabadiliko ya tabia nchi ili kuona namna ya kukabiliana nayo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk Amos Nungu ameeleza kuwa mada mbalimbali ziliwasilishwa kwenye kongamano hilo na mapendekezo yaliyotolewa ni kuimarisha midahalo ya wadau, kutekeleza sera ya viwanda kwa kushughulikia changamoto za sera hiyo na kuunganisha ushirikiano kati ya elimu ya juu na viwanda pamoja na kuunganisha sekta ya viwanda, sayansi na teknolojia.
Amesema kuna mapendekezo ya kuwa na teknolojia zitakazowasaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
”Costech imeombwa iratibu nyenzo au vifaa vya utafiti vitakavyotumiwa kwa pamoja na watafiti kutokana na gharama za juu za vifaa hivi, pia imeshauriwa kuwekeza teknolojia zenye gharama nafuu kuondoa hewa ukaa,” amesema Dk Nungu.
Pia imeshauriwa watafiti wajikite kufanya utafiti uchumi wa kibaolojia.
Naye, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi amesema nchi inahitaji maeneo ya sayansi, teknolojia na ubunifu yaweze kuimarishwa ili kukuza uchumi.
Amesema mijadala iliyojadiliwa kwenye kongamano hilo, ilijikita maeneo matano ikiwemo matumizi ya maarifa asilia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, uendelevu usalama wa chakula na kukuza sayansi, teknolojia na hisabati kwa uchumi stahimilivu na kuendeleza uchumi wa buluu wanahitaji wataalamu mahili kushika eneo hilo.
”Tutashirikiana kutekeleza maazimio haya kwa kushirikiana kati ya sekta ya umma na binafsi pamoja na kuweka utaratibu sahihi ili kutekeleza maazimio hayo na kupiga hatua,” amesema.
No comments