Breaking News

PROF. NAJAT: STEM NI MUHIMILI WA MAENDELEO NA UCHUMI

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) Prof. Najat Mohammed amesisitiza umuhimu wa kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi, hususan Hisabati na Fizikia, kama njia ya kukuza mafanikio ya teknolojia na maendeleo ya uchumi.

Akizungumza wakati wa mada Katika Kongamano la Tisa la Wanasayansi, Watafiti, na Wabunifu lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Prof. Najat alisema, "Tunapaswa kuchukua hatua za kuhakikisha wanafunzi wanapenda masomo ya sayansi, hususan Hisabati na Fizikia. Tunapaswa kuwahamasisha, kuwapa moyo, na kuhakikisha wanapata vifaa vinavyohitajika."

Aliendelea kueleza kuwa wahitimu wa masomo ya STEM (Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, na Hisabati) wana jukumu kubwa katika maendeleo ya Teknolojia na suluhisho la changamoto za kiuchumi na kijamii. Alisema, "Wahitimu wa STEM wanapaswa kuwa wasanifu wa mafanikio ya kiteknolojia, waanzilishi wa suluhisho endelevu, na waendeshaji wa ukuaji wa uchumi."

Prof. Najat pia alishauri serikali na sekta binafsi kushirikiana kuwekeza katika elimu ya STEM kwa kuboresha miundombinu, kuongeza walimu wa Sayansi, na kuhamasisha vijana, hususan wasichana, kujiunga na masomo hayo.

Kongamano hili limekusanya wataalamu kutoka sekta mbalimbali ili kujadili njia za kutumia sayansi na ubunifu kwa maendeleo endelevu. Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kwa Ustahimilivu wa Tabianchi na Uchumi Shindani."

Katika hitimisho la wasilisho lake, Prof. Najat alitoa wito kwa taasisi za elimu na wadau wa maendeleo kuhakikisha vijana wanapata mazingira bora ya kusomea STEM akisema, "Ili kufanikisha maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia, tunahitaji kizazi cha viongozi wa STEM wenye maarifa na ujuzi wa kubuni suluhisho za changamoto za dunia." 

No comments