Breaking News

VIONGOZI WA DINI WATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA RUAHA

Na. Jacob Kasiri - Ruaha.
Sifa za kipekee, nguvu na ujasiri unaotumiwa na Simba wakati wa kuwinda umekuwa na hamasa na shauku kubwa leo kwa viongozi wa dini kutumia zaidi ya dakika 30 wakimuangalia mnyama huyo aliyekuwa amelala kichakani baada ya kushiba huku pembeni kukiwa na masalia ya kitoweo baada ya mawindo yake.

Simba mara zote huchukuliwa kama mfalme wa nyikani akiwa na uwezo wa kuwinda wanyama wakubwa zaidi ya umbo lake, sifa inayowafanya watu kuwa na hamu ya kuwaona katika mazingira yao ya asili.

Akitoa mifano ya baadhi ya majina yanayoashilia sifa za mnyama Simba kama vile Simba wa Yuda, Askofu wa Kanisa la Orthodox Dimitrios Nziku alisema, “Nimefurahishwa sana nilipomuona Simba maana tulikuwa tumeshaanza kusinzia kwenye gari ila baada ya kuambiwa simba huyu hapa nilipata nguvu na kujisemea moyoni safari yangu imezaa matunda.”
Aidha, viongozi hao wa dini wamefurahishwa na mandhari nzuri na wingi wa wanyama waliokutana nao wakati wakitalii, hata hivyo wamesikitika kuona mto the Great Ruaha ukiwa na maji kidogo sana tofauti na wanavyousikia, hivyo wameahidi kuwa mabalozi wa kwenda kuusemea kwa waumini wao.

Akiwakaribisha viongozi hao wa dini, Afisa Mhifadhi Mkuu Neema Kaitira mkuu wa kitengo cha Ikolojia alisema, “Licha ya changamoto za upungufu wa maji katika mto huu, hifadhi imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha maji yanapatikana kwa wanyama ili kuinusuru ikolojia ya hifadhi hii.”

Hata hivyo, Muikolojia huyo aliongeza kuwa kwa mwaka huu kuna unafuu kidogo tofauti na mwaka jana kwani bado mto huu unaendelea kutiririsha maji, ni matumaini yetu mvua zinazotarajia kunyesha mwaka huu zitakutana na maji haya.

Ziara hiyo ya viongozi hao wa dini iliyofanyika leo tarehe 03.07.2024 ni mwendelezo wa maandalizi ya wiki ya maadhimisho ya miaka 60 ya Hifadhi ya Taifa Ruaha ambayo yatafanyika Oktoba 07, 2024 Msembe ndani ya hifadhi hiyo.



No comments