Breaking News

RAIS MWINYI AFUNGUA S!TE 2024, AMPONGEZA MHE. RAIS SAMIA, WIZARA KWA ONGEZEKO LA MAPATO YA UTALII

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, DKt. Hussein Ali Mwinyi, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa jitihada kubwa za kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya utalii katika kipindi kifupi cha Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Mwinyi amesema hayo wakati akifungua Onesho la 8 la Utalii la Kimataifa la Swahili (8th edition of the swahili international tourism expo – s!te 2024) lililoanza leo oktoba 11, 2024 katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es salaam ambalo limewakutanisha wanunuzi wa bidhaa za utalii, Waoneshaji, Wawekezaji na wadau mbalimbali wa utalii wa ndani na nje ya Tanzania.
“Kutokana na juhudi hizo za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, idadi ya watalii wa kimataifa wanaotembelea Nchi yetu imekua kwa kasi sambamba na ongezeko la mapato yatokanayo na sekta ya utalii. Mathalan, hadi kufikia mwezi Agosti, 2024 Tanzania imepokea jumla ya watalii wa kimataifa 2,026,378 ikiwa ni takwimu za juu kabisa kuwahi kufikiwa katika historia ya Nchi yetu. Pia, mapato yatokanayo na sekta ya utalii yamefikia Dola za Marekani bilioni 3.5”. amefafanua Mhe. Mwinyi

Amesema sekta ya utalii imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa Tanzania, huku ikichangia asilimia 17.2 ya Pato Ghafi la Taifa, asilimia 25 ya mauzo ya nje na kuzalisha ajira zaidi ya milioni 1.5 ikiwa ni ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kupitia mnyororo wake wa thamani. 
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yamewezesha nchi yetu kutambuliwa kimataifa na kupata tuzo mbalimbali ambapo taarifa iliyotolewa mwezi Septemba, 2024 na Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism – World Tourism Barometer) ambapo inaonesha kuwa, Tanzania imeshika nafasi ya 6 Duniani na ya kwanza Barani Afrika kwa kuwa na ongezeko kubwa la watalii.  

Miongoni mwa tuzo hizo ni zile zilizotolewa mwaka 2023 na World Travel Awards (WTA) ambao wameitambua Bodi ya Utalii Tanzania kama Africa’s Leading Tourist Board, Kisiwa cha Thanda Shunghumbili, Mafia kama World Leading Exclusive Private Island, Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro kama Africa’s Leading Tourist Attraction.


No comments