Breaking News

NIDA YABORESHA MCHAKATO UPATIKANAJI VITAMBULISHO

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),  Geofrey Tengeneza akifafanua jambo kwa na waandishi wa habari juu ya maboresho yaliyofanywa na mamlaka hiyo katika kitengo chake cha huduma kwa wateja (call centre) mazungumzo hayo yalifanyika katika ofisi za makao makuu ya NIDA Dar es salaam.

Dar es salaam
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imefanya maboresho katika kituo chake cha kutolea Huduma kwa Wateja (Call Centre) ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wenye uhitaji wa vitambulisho na huduma nyingine mbalimbali ili kuwaondolea usumbufu wa kulazimika kwenda  katika ofisi zake za wilaya na mikoa na kuokoa muda na gharama

Akiongea na waandishi katika Makao Makuu ya Nida jijini Dar es Salaam, Msemaji na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa mamlaka hiyo Geofrey Tengeneza amesema kuwa maboresho mbalimbali yamefanyika katika kituo hicho baada ya kuwekewa miundombinu ya kisasa na kuongeza idadi ya watoa huduma ili kuwafikia watu wengi na kwa urahisi tofauti na ilipokuwa hapo awali.

Kufuatia maboresho hayo, amesema kuwa namba zote za mitandao mbalimbali ya simu zilizokuwa zikitumiwa na wateja hapo awali hazitatumika tena ifikapo Oktoba 28 mwaka huu na badala yake namba itakayotumika ni 0232210500 ya mtandao wa TTCL pekee.

Kupitia namba hii, amesema wateja wataweza kupiga simu na kuuliza maswali mbalimbali kama vile kujua kama vitambulisho vyao vimekamilika, kutaka kujua namba zao za vitambulisho na mambo mengine .

Maboresho haya kwa mujibu wa Tengeneza ni katika sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, huku akiahidi maboresho zaidi katika kutoa huduma kwa wateja.

Mbali na maboresho ya kituo hicho cha huduma kwa wateja, Bw. Tengeneza  pia ametoa wito kwa wananchi kutumia mitandao mbalimbali ya kijamii ya Nida katika kupata huduma mbalimbali.

“Tunajivunia kuwafikia wananchi wengi zaidi kupitia mitandao ya kijamii na kupitia maboresho ya kidijitali yaliyofanyika katika kituo chetu cha huduma tunategemea kuwafikia waananchi wengi zaidi wakiwemo wale wanaoishi vijijini,” amesema.

Amesema wale watakaokuwa na maswali watapewa majibu ya papo kwa papo kutegemeana na maswali watakayoulizwa na mengine yatajibiwa na wakuu wa idara kutegemeana na uzito wake.

Amesema mpaka kufika mwezi Agosti mwaka huu, mamlaka hiyo imefanikiwa kutengeneza vitambulisho milioni 21.5 kwa watu walioomba na wenye sifa ambapo kati ya hivyo, milioni 20.7 tayari vimeshasambazwa na vitambulisho milioni 19.5 kati ya hivyo tayari vimewafikia walengwa, ambao ni wananchi waliofikisha umri wa miaka 18 na kuendelea. 

No comments