Breaking News

RC CHALAMILA AKABIDHI GARI 2 KWA WAKUU WA WILAYA YA KINONDONI NA TEMEKE

Katika kuimarisha huduma kwa wananchi Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe Albert Chalamila amekabidhi magari mawili aina ya Prado TX kwa wakuu wa wilaya za Kinondoni na Temeke ili kuwawezesha kuwafikia wananchi na kuwahudumia kwa urahisi.

Akizungumza leo Septemba 30,2024 Jijini Dar es salaam Mkuu wa Mkoa Mhe Albert Chalamila amesema lengo la magari yaliyotolewa na Rais ni kusaidia wakuu wa Wilaya kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo na kuimarisha huduma kwa wananchi hata nyakati za usiku hivyo amewataka kuyatumia kwa malengo yaliyokusudiwa
Aidha RC Chalamila amesema kuwa magari hayo pia yatasaidia kipindi cha uchaguzi wa Serikali ya Mitaa kwa mwaka huu pamoja na uchaguzi mkuu mwakani kwa kuwawezesha viongozi hao kufika kwenye maeneo mbalimbali.

Kwa upande wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es salaam Dkt Toba Nguvila wakati akitoa taarifa kuhusu magari hayo amesema Serikali ilitenga fedha za kununulia magari yatakayotumiwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ili kuimarisha huduma

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe Saad Mtambule na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe Sixtus Mapunda wameshukuru kwa kupata magari hayo na kuahidi kuwa yatakwenda kufanya kazi husika ya kuwafikia wananchi na kutatua migogoro mbalimbali


No comments