MRADI WA KABANGA NICKEL WAVUTIA UWEKEZAJI MKUBWA KUTOKA KAMPUNI ZA AUSTRALIA
Perth, Australia
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Kampuni ya madini ya BHP inayotarajia kuingia ubia na Kampuni ya Lifezone Metal kwa ajili ya kuwekeza nchini Tanzania katika mradi wa uchimbaji madini aina ya Nickel,Wilayani Ngara Mkoa wa Kagera.
Mazungumzo hayo yalijikita katika kutoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa Kabanga Nickel unaosimamiwa na Kampuni ya ubia ya Tembo Nickel ambayo serikali pia ni mwanahisa.
Mradi wa Kabanga Nickel unatazamia kugharimu kiasi cha Dola za Marekani Bilioni 2.2 ambapo zaidi ya Dola Bilioni 1.6 zitatumika kwa ajili ya shughuli za ujenzi wa mgodi na uchenjuaji wa madini utakaofanyika wilayani Ngara,Kagera na Dola Milioni 600 zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha usafishaji wa madini (Multi-metals Refinery Facility) ambacho kitajengwa katika ukanda maalum wa kiuchumi (Special Economic Zone) eneo la Buzwagi, Wilayani Kahama, Shinyanga.
Kampuni ya BHP ni moja kati ya kampuni kubwa 3 za madini Duniani ambayo ina mapato Dola Bilioni 60 kwa mwaka sawa na Tsh Trilion 160 kwa mwaka.
Kampuni ya BHP inayotazamia kuingia makubaliano ya ubia na kampuni ya Life Metals kuendeleza mradi wa Kabanga, ilifunga shughuli za uchimbaji madini Barani Afrika miaka 15 iliyopita na sasa wapo tayari kurejea Afrika kupitia nchi ya Tanzania.
Waziri Mavunde alitumia fursa hiyo kuwashukuru kwa kuiamini Tanzania na kuamua kurudi kuwekeza kupitia mradi wa Kabanga na kuwahakikishia kwamba ni maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuendelea kuwavutia wawekezaji kwa kutengeneza mazingira wezeshi ambayo yamejengwa kwa weledi kupitia falsafa yake ya 4R.
Aidha pia Waziri Mavunde ambaye aliongozana na Balozi Baraka Luvanda Balozi wa Tanzania nchini Japan ambaye pia anasimamia Australia, ametembelea kujionea teknolojia itakayotumiwa kwenye ujenzi wa kiwanda cha kusafisha madini yaani _Multimetal Refinery facility_ ambayo itatumia teknolojia ya kisasa ya Hydrometallurgy kupitia Kampuni ya Tembo Nickel inayomiliki mgodi wa Kabanga nickel uliopo Ngara.
No comments