CUF YALAANI MAUAJI YA MHE. ALI MOHAMED KIBAO MJUMBE WA SEKRETARIETI KUU CHADEMA
CUF- Chama Cha Wananchi kimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya kuuawa kwa Mjumbe wa Sekretarieti Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mhe. Ali Mohamed Kibao ambaye awali aliripotiwa kushushwa kwenye basi maeneo ya Tegeta na watu walioaminika kwamba ni askari, na baadae mwili wake kuokotwa akiwa ameshauawa.
Matukio ya watu kupotea na hatimae kukutwa wameuawa yanaanza kuongezeka kwa kasi nchini hususan baada ya kusikika kwa baadhi ya viongozi wa CCM wakiwaambia hadharani askari Polisi kwamba wataanza kupoteza watu na kwamba jeshi la Polisi lisihangaike kuwatafuta wanaopotea. Hali hii imeanza kutengeneza hofu na kuirudisha nchi kwenye maisha ya taharuki licha ya matamko mbalimbali ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ya ndoto ya kuwarudisha watanzania kuishi pamoja kwa upendo na kuaminiana.
CUF- Chama Cha Wananchi kinalaani mauaji haya na matendo ya utekaji kwa ujumla na kinatoa wito kwa vyombo vinavyohusika kuhakikisha waliohusika kufanikisha unyama huu kwa namna moja ama nyingine wanakamatwa na kuchukuliwa hatua muafaka za Kisheria. Tunatoa pole kwa familia ya marehemu Ali Mohamed Kibao, CHADEMA na wote walioguswa na msiba huu wa kuhuzunisha. Aidha, tunamuombea marehemu Mafikio Mema na msamaha kwa Mwenyezi Mungu.
HAKIKA SOTE NI WA ALLAH NA KWAKE TUNAREJEA!
HAKI SAWA KWA WOTE!
Eng. Mohamed Ngulangwa
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma CUF - Chama Cha Wananchie
Septemba 8, 2024
No comments