Breaking News

RC CHALAMILA AONGOZA KIKAO CHA TATHMINI YA LISHE - DSM

-Asema lishe bora ni muhimu kwa ustawi wa jamii hapa Nchini.

-Awataka wadau kushirikishana na serikali kuwekeza katika afua za lishe ili kupunguza idadi ya watoto wenye upungufu wa damu.

-Asisitizia jamii kuchukua tahadhari kwa kujikinga na maradhi.

Dar es salaam 
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Albert Chalamila Leo Agosti 20,2024 ameongoza kikao Cha tathmini ya lishe katika ngazi ya mkoa katika Ukumbi wa Anartoglo- Ilala, kwa lengo la kujadili changamoto na mafanikio yaliyopatikana katika jitihada za kuboresha hali ya lishe mkoani humo hususani kwa watoto na wanawake wajawazito.

RC Chalamila amepongeza serikali chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kulipa kipaumbele suala la lishe na kusaini mkataba wa utekelezaji wa afua za lishe na Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa yote 26 ili kuwapima utendaji kazi wao katika kusimamia utekelezaji wa makubaliano yaliyowekwa na kuagiza idara zote na sekta zote kulichukulia suala Hilo kwa uzito wake.

Aidha RC Chalamila alisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka na za makusudi katika kuboresha lishe, akieleza kuwa tatizo la udumavu bado ni changamoto kubwa inayokabili jamii. Aliwahimiza viongozi wa wilaya na wakuu wa idara kushirikiana kwa karibu zaidi na wadau wengine kuhakikisha mipango iliyopo inatekelezwa kwa ufanisi.

Vilevile Mhe. Chalamila ameendelea kuikumbusha jamii kuchukua tahadhari kwa lengo la kujikinga na maradhi kama vile kufanya usafi binafsi na usafi wa Mazingira pamoja na afua za Kinga dhidi ya UKIMWI,Kifua kiku,Malaria na Magonjwa yasiyoambukiza pamoja na ufanyaji wa mazoezi ya viungo vya mwili.
Sanjari na hilo Katibu Tawala wa Mkoa Dkt. Toba Nguvila ametoa rai kwa wadau wa maendeleo kuwa waangalizi juu ya vyakula na mwenendo wa Clinic kwa kinamama wajawazito na kupinga matumizi ya pombe pamoja na madawa ya kulevya ili kuepusha athari kwa mtoto

Mwisho, kikao kilihitimishwa kwa makubaliano ya kuimarisha mikakati ya lishe kwa kushirikiana na wadau wote muhimu, huku wakilenga kuboresha zaidi utoaji wa huduma za lishe katika vituo vya afya na katika ngazi za halmashauri.


No comments