Breaking News

MTANZANIA EDHA NAHDI ANUNUA KIWANDA CHA CEMENT KENYA.

Mmiliki wa kampuni za Mbeya Cement na Camel, Edha Nahdi, amenunua kampuni kubwa zaidi ya saruji nchini Kenya kwa thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 260. 

Ununuzi wa kampuni hiyo ya Kenya, Bamburi Cement, inayojulikana kwa uzalishaji wa saruji ya tembo umefanywa kupitia kampuni ya AMSONS Group ambayo Nahdi ni Mkurugenzi Mtendaji.

Ununuzi huo wa kampuni ya Bamburi ambayo ina viwanda viwili kwenye miji ya Nairobi na Mombasa, utaifanya kampuni ya AMSONS kuwa mojawapo ya wawekezaji muhimu zaidi kwenye sekta ya saruji kwenye eneo la Afrika Mashariki.
Bamburi kwa sasa inazalisha wastani wa tani milioni 3.2 za saruji kwa mwaka na ukijumlisha na uzalishaji wa tani milioni 1.6 ambazo tayari zinazalishwa na AMSONS kupitia Mbeya Cement na Camel, uwezo wa kuzalisha saruji wa kampuni hiyo kwa sasa utafikia kiasi cha tani milioni 4.8 za saruji.
 
Hatua ya AMSONS kuingia kwenye biashara kwa kiwango hiki ni miongoni mwa hatua mpya kabisa kwenye uhusiano wa kiuwekezaji baina ya nchi za Afrika Mashariki. Kwa kawaida, wawekezaji kutoka Kenya wamekuwa wakiwekeza Tanzania kwa muda mrefu sasa lakini ununuzi huu wa Bamburi unaonyesha namna wawekezaji Watanzania wanavyoanza kuteka kibiashara nchi hiyo jirani.
  
Kampuni ya AMSONS ilianzishwa mwaka 2006 ikijulikana zaidi kwa biashara ya mafuta kupitia jina la Camel Oil lakini sasa imeingia kwenye biashara mbalimbali ikiwemo ya uzalishaji wa unga wa ngano na usafirishaji.
 
Vyombo vya habari vya Kenya na hasa kwenye mitandao ya kijamii vimeeleza kwamba jambo kubwa katika uwekezaji wa AMSON kununua kampuni ya Bamburi ni namna ilivyokubali kulipa gharama za ziada ili kufanikisha kukamilika kwa biashara hiyo.

No comments