Breaking News

HOJA 14 ZA PROF. BENGESI AKITOA UFAFANUZI WA HOJA ZILIZOIBULIWA NA WAZALISHAJI WA SUKARI NCHINI

Profesa Keneth Bengesi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, leo Julai 5, 2024 amezungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam, kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizoibuliwa na wazalishaji wa Sukari, pamoja na kueleza sababu za bei ya sukari kuwa juu kwa miezi kadhaa iliyopita. Miongoni mwa mambo aliyozungumza ni haya yafuatayo;

1. Mpaka sasa wazalishaji hawajawahi kuwasilisha Serikalini vikwazo wanavyolalamikia. Serikali ipo tayari kwa majadiliano. 

2. Mabadiliko ya sheria yamelenga kuwezesha bei ya sukari isiyomuumiza mwananchi, upatikanaji wa uhakika wa sukari muda wote, uwazi kwenye usambazaji wa sukari, Tathmini ya ufanisi wa viwanda vya sukari.

3. Msimamo wa Serikali kwenye Sukari ni Kuwalinda wananchi, Kuwalinda wakulima, wawekezaji na wadu wengine wa sukari, Kuendeleza majadiliano na wadau kutatua changamoto na kuikuza sekta ya Sukari

4. Si kweli kwamba wazalishaji wa sukari nchini walicheleweshwa kupewa vibali, isipokuwa wao ndiyo walichelewa kuchukua vibali na kuingiza sukari nchini. 

5. Msimu wa 2022/23, Kampuni nne za wazalishaji walichukua vibali vya kuagiza sukari, ila ni kiwanda kimoja tu cha Kilombero ndicho kilichoingiza sukari kwa msimu huo kiasi cha tani 2,380. Viwanda vingine vyote havikuingiza sukari nchini. 

6. Kushindwa kwa wazalishaji kuingiza sukari katika msimu wa 2022/2023 kuliwapotezea sifa ya kisheria ya kupewa vibali kwa msimu wa 2023/2024. Hata hivyo Serikali iliendelea kuwapa vibali. 

7. Kitendo cha wazalishaji kutoingiza kiasi chote cha sukari kilichoidhinishwa 2022/23 kilisababisha upungufu wa sukari na kupanda bei hadi kufikia shilingi 4,000 kwa kilo moja mwezi Juni, 2023.

8. Kampuni ambazo zimebezwa na kuitwa “kampuni za vocha” ndizo zilizoingiza sukari nchini kwa haraka katika kipindi kigumu cha upungufu mkubwa, na hivyo kusaidia kushusha bei ya sukari kwa wananchi.  

9. Serikali kupitia vyombo vyake vya Ulinzi na Usalama pamoja na Mamlaka za Udhibiti hufanya ukaguzi wa sukari yote inayoingizwa nchini kupitia Bandari na mipaka yote nchini ili kuhakikisha usalama wake kwa watumiaji.

10. Sukari iliyoingia nchini, ubora wake sio wa kutiliwa shaka kwa kuwa huhakikiwa na TBS hapa nchini kabla ya kuiruhusu kusambazwa kwa walaji. Hivyo mtu yeyote anayetaka kujiridhisha na ubora na usalama wa sukari iliyoingizwa nchini anaweza kuona nakala za cheti cha ithibati (certificate of conformity) na vipimo vya maabara vya TBS. 

11. Kwenye msamaha wa kodi, lengo la Serikali halikua kuzinufaisha kampuni zilizoagiza sukari bali ilikua ni kumlinda mlaji wa mwisho kwa kupunguza makali ya bei ya sukari kipindi cha uhaba.

12. Mahitaji ya sukari nchini ni takribani tani 650,000 kwa mwaka ikijumuisha sukari ya dharura (buffer stock) ya matumizi yasiyopungua miezi miwili na sio tani 490,000 kama ilivyowasilishwa na wazalishaji

13. Mahitaji ya sukari nchini ni takribani tani 650,000 kwa mwaka ikijumuisha sukari ya dharura (buffer stock) – na sio tani 490,000 kama ilivyowasilishwa na wazalishaji.

14. Serikali inawalinda wazalishaji wa ndani kwa namna mbalimbali ikiwemo misamaha ya kodi, kuwapatia ardhi, kuwajengea miundombinu ya barabara, umeme, madaraja, n.k. ili kuwawekea mazingira bora ya uzalishaji na ushindani wa soko.

No comments