Breaking News

ACT WAZALENDO WAITAKA SERIKALI KUSITISHA MPANGO WA KUWAONDOA MACHINGA K.KOO NA MAENEO MENGINE

Waziri kivuli wa Viwanda na Biashara. Ndg. Mwanaisha Zuberi Mndeme

Kauli ya Rais Samia ni tangazo la Operesheni ya kuwaondoa wamachinga nchini.

Chama cha ACT Wazalendo kinaitaka Serikali kuondoa vikwazo na kusitisha mara moja mipango na operesheni za kuwaondoa wamachinga Kariakoo na maeneo mengine mijini.  Tunaungana na wafanyabiashara wadogo nchini katika kipindi hiki cha sherehe za sabasaba kupigania mazingira rafiki ya kibiashara kwa wamachinga ili kutumia maeneo mbalimbali ya miji katika kujipatia kipato na kuinua maisha yao.

Wamachinga wamekuwa waathirika wakubwa wa mipango ya Serikali kila inapojaribu kushughulikia matatizo ya Wafanyabiashara nchini. Wamachinga wamekuwa wakiondolewa, wakinyang’anywa mali zao, wakivamiwa na migambo mara kwa mara na miaka ya hivi karibuni masoko yao yakiunguzwa moto.

Wasiwasi tulioueleza kutokana ya madai ya wafanyabishara wa Kariakoo katika mgomo wa hivi karibuni ulitaja wamachinga kuwa ni kero na kikwazo katika biashra zao. Tulieza kuwa madai hayo ni kuwatoa kafara wamachinga na kuwaweka katika hatari zaidi ya kuondolewa kwa nguvu na kunyimwa haki ya kutumia miji na majiji kujipatia kipato.

Ni wazi sasa Serikali inaenda kuteleza kwa nguvu zote baada ya kauli ya Rais Samia Suluhu ya kuliagiza Jeshi la Polisi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Waziri wa Viwanda na biashara kuwapanga wamachinga Kariakoo na maeneo mengine nchini. 

ACT Wazalendo tupinga vikali baraka hizi za Rais Samia kwa kuwa uhalisia na uzoefu unaonesha kuwa kinachoenda kutekelezwa ni kuondolewa katika maeneo yao ya asili ya kibiashara (natural markets). Kauli hii ni tangazo la operesheni ya fukuza fukuza ya wamachinga ambayo kwa miaka yote inaishia, kuwaumiza, kuwafukarisha na kuleta hasara kubwa kwa wananchi hawa.

Serikali imekataa kabisa kujifunza katika operesheni zote ilizoziendesha kuwa na mtazamo mpya wa namna miji yetu inavyopaswa kuwa ili kuakisi mahitaji ya jamii tuliyonayo leo na tunayotamani kuijenga? Serikali haitaki kuangalia upya mipango ya miji na matumizi ya maeneo yote ya wazi ili kuweka mazingira wezeshi ya kibiashara na ustawi wa wamachinga nchini? 

Mwisho, ACT Wazalendo itaendelea kuhakikisha inazuia ukandamizaji, kuhamishwa na kuondolewa kwa wamachinga mijini na katika masoko yao ya asili kama vile maeneo yenye mzunguko mkubwa wa watu (hub market). Tunawasihi Wamachinga kuwa na umoja na mshikamano katika wakati huu mgumu ambao Serikali ya CCM imekusudia kuwaondoa kwenye maeneo yao ya biashara.  

Imetolewa na;
Ndg. Mwanaisha Zuberi Mndeme
Waziri kivuli wa Viwanda na Biashara.
07 Julai 2024.

No comments