Breaking News

WALIOHAMIA MSOMERA KUTOKA NGORONGORO WAISHANGAA MISA

Baadhi ya wananchi wa jamii ya kimasai nchini Tanzania wameshangaa kile walichosema  kauli ya uzushi iliyotolewa na taasisi  inayoitwa Masaai International Solidarity Alliance -MISA kwa kuainisha madai mbalimbali yaliyotolewa na shirika hilo lisilo la kiserikali na kuyaita kwamba madai hayo ni ya kipuuzi.

Baadhi ya wananchi hao wa jamii hiyo inayoishi nchini Tanzania waliohama kwa hiyari na kwenda kuishi katika Kijiji cha Msomera mkoani Tanga wamesema kuwa madai yaliyotolewa na jumuiya hiyo huenda yametolewa na wamasai ambao hawaishi Tanzania na hawana uchungu na wenzao ambao wananchi Tanzania hasa ukizingatia kuwa wana uhuru mkubwa wa kuhama na mifugo yao mahali popote nchini.

Wakizungumza na  mwandishi wetu katika Kijiji cha Msomera  baadhi ya wananchi hao  wamesema taasisi hiyo  imeandaa madai ya uzushi ambayo wao kama wananchi wanaona kwamba pengine yametolewa  kwa nia ovu  na kjuitaka taasisi hiyo kufika Msomera na kuzungumza na wananchi ili kupata ukweli badala ya kuzusha taarifa ambazo hazina mantiki yoyote. 

“Inavyoonekana MISA inaundwa na wamasai kutoka nchi nyingine duniani na si Tanzania kwani sisi wamasai tunaoishi Tanzania hatubughudhiwi na mtu yoyote yule ndiyo maana kila sehemu ya nchi hii tupo tukifanya shughuli zetu za ufugaji hivyo wasitutumie kutafuta fedha”,alisema  Joseph Supuk mwananchi aliyehama kutoka Ngorongoro na sasa  anaishi katika Kijiji cha Msomera.

Bwana Luca Tiamasi mmoja wa wananchi waliohamia katika Kijiji cha Msomera amesema aliposikia taarifa za taasisi hiyo kwenye mitandao ya kijamii alistuka kwani katika zoezi hilo hakuwahi kuona jeshi lolote likishiriki katika kuwahamisha na badala yake wengi wao wamekuwa wakiomba wenyewe kuhama baada ya kupata hamasa kupitia kwa wahamasishaji na vyombo vya habari.

Naye Sindato  Mollel kutoka katika Kijiji cha Endulen wilayani Ngorongoro aliiomba taasi si hiyo kuacha kupotosha kwani jamii ya wamasai wanaotoka ndani ya hifadhi ya Ngorongopro hawajawahi kulazimishwa kuhama katika eneo hilo bali wamevutiwa kufanya hivyo kutokana na mazingira mazuri ya Kijiji cha Msomera ukilinganisha na walipokuwa wanaishi awali.

Wakijibu hoja za shirika hilo la MISA viongozi hao wananchi hao wamesema taasisi hiyo imetangaza kuporwa kwa ardhi ya wamasai nchini Tanzania ambao wamesema madai hayo wanayapinga kwa sababu hakuna mmasai yoyote ambaye ameporwa ardhi kwani Tanzania ni nchi yenye ardhi ya kutosha kulinganisha na maeneo mengine duniani.

“Kama nchi zao hazina ardhi waje na wafuate taratibu wa kuwa raia  ili tuwapatie ila wasisingizie kwamba sisi wamasai wa Tanzania tuna shida ya ardhi,tunafuga mifugo yetu kuanzia Arusha mpaka Dare ssalaam,tunaelekea lindi,Mtwara hadi Ruvuma na wala hakuna mtu yoyote anayetubughudhi wasitake kutumia migongo yetu kupata fedha kutoka kwa wafadhili”.alisema mwananchi huyo
 .
Wananchi hao  wamesema kuwa taasisi hiyo ya MISA inatumika kwa maslahi ya watu wachache  na ndio maana haiwezi kuja kuzungumza changamoto ya jamii ya kimasai ndani ya Tanzania na matokeo yake wamekuwa wakizunguka katika nchi mbalimbali duniani kutafuta misaada ili waweze kutumia fedha hizo kwa maslahi yao na familia zao.

“Kama kweli wana uchungu na wamasai wa Tanzania waje waone namna sisi tunavyoishi na wasitumie majina yetu katika kujinufaisha kiuchumi  kwani Tanzania hatuna matatizo ya kufanya shughuli zetu kutokana na mifumo mizuri iliyowekwa na serikali yetu katika umiliki wa ardhi na tumekuwa tukihama kadri tunavyotaka wenyewe”, alisema Moses Laizer mmoja wa wananchi aliyehamia Msomera.

Kuhusiana na zoezi linaloendelea la kuwahamisha wananchi kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kwenda Msomera viongozi hao wa jamii ya wamasai wamesema suala hili linafanyika bila kutumia nguvu yoyote na wananchi wa jamii hiyo wamekuwa wakielimishwa na kuondoka kwa hiyari ndani ya hifadhi hiyo ambayo kwa sasa imezidiwa na wingi wa watu,mifugo na shughuli za kibinadamu.

Jamii ya wamasai  nchini Tanzania ipo kwenye mikoa yote wakifanya shughuli zao za ufugaji na wamekuwa wakihama na mifugo yao kutoka sehemu moja ya nchi hadi nyingine na hivi sasa wamekuwa wakihamia katika visiwa vya Zanzibar ambapo wanaendelea na shughuli zao bila kubughudhiwa na mamlaka kwani kwa mujibu wa katiba ya Tanzania mtu ana uwezo wa kuishi popote bila kubughudhiwa na mtu.

Kutokana na matamko hayo ya jumuiya hiyo jamii hiyo inaona kwamba ni kama inataka kuwachonganisha na serikali na jamii nyingine za kitanzania na hivyo kuamua kupaza sauti zao kwa jamii ya kimataifa ili ielewe kwamba pengine  MISA ni taasisi inayoundwa na wamasai wanaotoka katika mataifa mengine  duniani.
Kwa mujibu wa maelezo kutoka serikali ya Tanzania mpaka sasa hakuna nguvu yoyote inayotumika katika kuhamisha watu katika maeneo ya nchi bila kufuata taratibu na kwa mujibu wa sheria za Tanzania ardhi ni mali ya Rais na pale anapoamua kuwa ardhi hiyo itumike kwa kazi nyingine kuna taratibu ambazo zimekuwa zikifuatwa.

Aliyekuwa Msemaji Mkuu wa serikali ya Tanzania Mobhare Matinyi  hivi karibuni amenukuliwa akiwaambia waandishi wa habari kuwa serikali ya Tanzania itaendelea kuheshimu haki za binadamu katika utekelezaji wa  zoezi la kuhama watu kwa hiyari na hakuna mwananchi atakayeshurutishwa kufanya  hivyo.

Matinyi alisistiza kuwa serikali imejipanga vizuri kuhakikisha wananchi wanaokubali kuhama kwa hiyari wanalipwa stahiki zao za kisheria lakini pia alisisitiza kuwa kwa wale ambao wataendelea kubaki ndani ya hifadhi hiyo wataendelea kuelimishwa kuhusiana na zoezi hilo na serikali haitositisha huduma yoyote mpaka zoezi hilo litakapokamilika.

Kwa muda mrefu jamii ya kimaisai nchini Tanzania imekuwa ikiishi kwa amani na imekuwa ikiruhusiwa kufanya shughuli zake za ufugaji katika eneo lolote lile kulingana na sheria zilizotenga maeneo hayo na katika siku za hivi karibuni jamii hiyo ya kimasai imekuwa ikishawishiwa na watu wanaotafuta fedha kubaki katika maeneo yenye wanyama wakali ili taasisi kama MISA wawatumie kupata fedha.

 

No comments