Breaking News

TAMASHA LA WEST KILI FOREST TOUR CHALLENGE LAFANA

Siha
Mamia ya wananchi wa wilayani Siha pamoja na wageni kutoka nje na ndani ya nchi wameshiriki Tamasha la West Kili Forest Tour Challenge ambalo linalenga kukuza utalii endelevu, kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, na kuleta pamoja wadau kutoka sekta mbalimbali ili kujifunza na kushirikiana kwa manufaa ya jamii na mazingira.

Tamasha hilo lililofanyika ndani ya Shamba la Miti la West Kilimanjaro, linalosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania -TFS limedumu kwa siku mbili Jumamosi na Jumapili (Juni 22-23, 2024) limewavuta wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi kujifunza na kuhamasisha shughuli za uhifadhi, na kufurahia matunda ya uhifadhi kupitia utalii ikolojia.
Mkuu wa Wilaya Siha mkoani Kilimanjaro Mhe. Dkt. Christopher Timbuka amesema tamasha hilo linalofanyika kila mwaka lililohusisha michezo mbalimbali kama vile mbio za baiskeli, waendesha pikipiki, uchoraji pamoja na mbio fupi limelenga kuwaleta watu pamoja kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na utalii wa ndani katika misitu ya West Kilimanjaro.

“Kupitia michezo inaweza kuwa njia rahisi kuhamasisha utalii na uhifadhi wa mazingira, niwatakie kila la kheri katika zoezi hili mnapokwendwa kulianza lakini ‘take your time, hatushindani, tunashiriki, alisema Mhe. Dkt. Timbuka.

Awali Mratibu wa Tamasha la West Kili Forest Tour Challenge 2024, Mhifadhi Mensieur Elly alisema mashindano ya michezo yanayofanyika katika tamasha hilo sio mashindano kama yanayofanyika sehemu nyingine bali ni adventure.
"Ndugu zangu wanariadha, waendesha baiskeli, waendesha pikipiki, wale watakaoshiriki matembezi hifadhini na watakaoshindana kuogelea kwenye swimming pool ya asili, mkumbuke hii ni adventure, take your time, enjoy as you can, sote tutapata medali na zawadi kwa baadhi yetu,” alisema Mhifadhi Elly.
 
Kwa upande wake Mhifadhi Msaidizi Shamba la Miti West Kilimanjaro, Godfrey Baraka amesema Shamba la Miti West Kilimanjaro limekuwa likifanya tamasha hilo kwa mafanikio kwa misimu minne sasa, na kutoa wito kwa wadau kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika msitu wa kupandwa na asili wa shamba hilo.


No comments