Breaking News

IPTL KULISHTAKI GAZETI LA MWANAHALISI

Mwanasheria wa IPTL, bwana Leonard Manyama 

Dar es salaam;
Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imeeleza kusudio lake kuwashtaki wamiliki, wahariri pamoja na wachapishaji wa Gazeti la MwanaHALISI iwapo hawataomba radhi kwa kile ilichodai upotoshaji uliofanywa gazeti hilo dhidi ya IPTL.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Aprili 28 na Wakili wa IPTL, Leonard Manyama inaeleza kuwa hatua hiyo ya kuishtaki MwanaHALISI itafanyika kama uongozi wa gazeti hilo utashindwa kuomba radhi, kukanusha habari hizo na kulipa fidia kama barua ya IPTL iliyowasilishwa kwa wadaiwa kupitia mawakili wake inavyowataka.

Taarifa hiyo iliyotolewa na uongozi wa IPTL kupitia Wakili Manyama inadai kuwa gazeti MwanaHALISI kwa nyakati tofauti limekuwa likiandika habari za kuupotosha umma dhidi ya IPTL, huku ikitaja moja ya habari hizo zilizochapishwa na gazeti hilo kuwa ni ya Aprili 18 mwaka huu.

IPTL imedai katika toleo hilo, gazeti hilo liliandika habari yenye kichwa kisemacho ‘Dili IPTL Laiva: Nyaraka zanyofolewa kumbeba Singasinga, Sasa kuchotewa zaidi Sh trilioni 1.8’ jambo ambalo IPTL inadai ni uongo.

Wakili Manyama amesema katika taarifa yake hiyo kwamba Aprili 4, 2024 gazeti la MwanaHALISI liliandika habari yenye kichwa ‘IPTL rushwa tupu: Siri za kutaka kumlipa mabilioni mengine Singasinga zaiva," imebainisha taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo pamoja na mambo mengine,imeelezwa kuwa IPTL ilianzishwa kwa ajili ya kuzalisha umeme wa Megawati 100 na kuliuzia Shirika la umeme, TANESCO. 

Imesema kuwa ili kufanikisha lengo hilo IPTL ilisaini Mikataba mitatu kati yake na TANESCO pamoja na Serikali, Mikataba hiyo ilikuwa kwa ajili ya kununua umeme.

Kwa mujibu wa Mikataba hiyo, TANESCO ilitakiwa kununua umeme wote unaozalishwa na mitambo ya IPTL iliyopo Tegeta, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam na kulipia malipo ya nguvu ya umeme.

Pia Serikali ilitakiwa kuhakikisha kuwa kama TANESCO inashindwa kulipa malipo hayo, basi Serikali inalipa na kuhakikisha kuwa leseni zote na vibali vyote vinavyohitajika ili IPTL izalishe umeme, vinapatikana bila kikwazo chochote.

Mwaka 1997 IPTL ilikopa fedha za Ujenzi wa Mitambao ya IPTL kutoka Benki Nne za Malaysia ambazo ni Bank Bumiputra Malaysia Berhad, Sime Bank Berhad, BBMB International Bank (L) Ltd na SIME International Bank (L) Ltd.   

Mikataba hiyo ya Kununua Umeme ilikuwa ya muda wa miaka 20 kuanzia tarehe ambayo IPTL itaanza kuzalisha na kuuzia umeme TANESCO ambapo Mikataba hiyo ilianza Januari 15, 2002 na hivyo ilitakiwa kusitishwa Januari 15, 2022