Breaking News

DARAJA LA TANZANITE KUFUNGWA KILA JUMAMOSI KUPISHA MAZOEZI

Na WAF - Dar Es Salaam 
Barabara inayoanzia Taasisi ya Saratani Ocean Road kupitia Hospitali ya Aga Khan hadi kwenye daraja la Tanzanite itafungwa kila siku ya Jumamosi kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:00 asubuhi kwa ajili ya kupisha mazoezi yatakayo saidia kupunguza magonjwa Yasiyoambukiza. 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ametoa maelekezo hayo leo Aprili 28, 2024 baada ya kumaliza mbio za KM 5 za ‘Run 4 Autism’ (watoto wenye Usonji) zilizoanzia katika viwanja vya farasi kupitia daraja la Tanzanite Jijini Dar Es Salaam yenye lengo la kuchangia watoto wenye Usonji nchini Tanzania. 
“Suala hili sio geni, ni sisi Tanzania ndio tulikua hatujaanza, tumeona nchi nyingi kubwa zinafunga barabara kwa muda  ili kuruhusu watu kufanya mazoezi ya kukimbia na kutembea kwa uhuru mkubwa.” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa 

Amesema, vyombo vitakavyoruhusiwa muda huo ni magari ya wagonjwa wa dharula (Ambulance) ambayo yataratibiwa na Mkuu wa Wilaya, baiskeli za mazoezi pamoja na pikipiki itakayotumika kumbeba mpiga picha kwa kibali maalum, wengine watapita barabara nyingine kwa muda huo. 

“Mimi nimeshiriki marathon mara nyingi hapa Dar Es Salaam, nimeona wananchi wanavyojitokeza kwa wingi kufanya mazoezi ya viungo na kukimbia, wazee kwa vijana baada ya kupata elimu iliyosababisha kuhamasika kufanya mazoezi hivyo lazima kuwawekea mazingira rafiki ili wafanya mazoezi kwa uhuru.” Amesema Majaliwa 

Awali  Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu aliiomba Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu kufungwa kwa barabara hiyo ili kuwapa uhuru watu wanaofanya mazoezi ya viungo, kukimbia na kutembea wafanye kwa uhuru. 

“Mhe. Waziri Mkuu kama itakupendeza tunaomba barabara hii ya Tanzanite kila Jumamosi ifungwe kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:00 asubuhi ili wa muda huo iweze kutumika kwa ajili ya mazoezi.” Ametoa ombi hilo Waziri Ummy.