Breaking News

ZOEZI LA UGAWAJI CHANJO HPV LAFIKIA ASILIMIA 95

Dar es Salaam 
Hadi kufikia Aprili 27, 2024 tayari zoezi la Ugawaji wa chanjo ya dozi moja ya HPV imewafikia ya asilimia 95 ya mabinti wenye umri wa miaka 9 hadi 14 wa Tanzania bara na visiwani tangu kuanza kutolewa kwake Aprili 22, 2024.

Hayo yamesemwa na Meneja Mpango wa Taifa wa Chanjo Dkt. Florian Tinuga wakati wa Semina kati ya wanahabari wa Mkoa wa Dar es Salaam na waratibu wa chanjo kutoka wizara ya Afya, Semina iliyofanyika Aprili 27, 2024, kwakulenga kutoa elimu kuhusu Chanjo ya HPV.

Dkt. Tinuga amesema lengo lao ni kuwafikia mabinti Millioni tano wa Tanzania nzima ambapo mpaka sasa zoezi hilo limeonyesha mafanikio makubwa ikiwa ni wiki moja tu tangu kuanza kwake.

"Tulipoanza zoezi siku ya Jumatatu tulilenga kufikia watoto wenye umri wa miaka 9 hadi 14 takribani milioni tano na kwa tanzania nzima bara na visiwani ambapo kwa bara ni takribani milioni nne na laki nane, na wengine waliobaki Zanzibar, ila hadi kufikia tarehe 27, Aprili 2023 tumefikia walengwa kwa asilimia 95" amesema Dkt. Tinuga.

Dkt. Tinuga ameongeza kuwa kufanikiwa kwa Lengo hilo kumetoka na maamuzi ya kufanya mabadiliko ya kutoa dozi moja sahihi na kuweza kuwafikia mabinti wengi zaidi ambapo kwa siku ya kwanza pekee walichanja asilimia 27 huku lengo likiwa kila siku kuchanja asilimia 20.

Dk Tinuga ameongeza kuwa wasichana wenye umri wa Miaka 9-14 wapatao 5,028,357 kwa Bara na &Visiwani, ikiwa bara ni 4,841,298 na 187,059 Visiwani watafikiwa na chanjo hiyo kwa Mikoa 31 na Halmashauri 195 kabla ya kufikia hatamu Disemba mwaka huu.

“Chanjo ni salama na hutolewa bure kwa walengwa kwa hiari na chanjo hiyo hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya mlango wa kizazi inapatikana katika vituo vya kutolea huduma za chanjo na hutolewa vituoni ,kwenye jamii na shuleni na hutolewa wakati wa kampeni na kawaida,” amesisitiza Dk Tinuga.