PINDA AKAGUA ENEO WATAKAPOHAMISHIWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO HANANG
MANYARA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda ametembelea na kukagua eneo limepimwa viwanja kwa ajili ya kuhamisha waathirika wa Mafuriko yaliyotokana na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang.
Mhe Pinda amefanya ukaguzi huo tarehe 5 Januari 2024 akiambatana na mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga pamoja na viongozi wengine wa mkoa pamoja na wa wilaya ya Hanang.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeshiriki pamoja na na wadau wengine katika zoezi la kutathmini kiwango cha uharibifu uliotokana na maafa yaliyotokea tarehe 3 Des 2023 na kushauri juu ya maeneo yanayoweza kutumika kuhamisha waathirika.
Akiwa katika eneo hilo tarehe 5 Januari 2024 wilayani Hanang mkoani Manyara, Mhe Pinda alielezwa na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Manyara Wenceslaus Mtui kuwa, jumla ya ekari 100 kutoka Jeshi la Magereza kwenye eneo la Warret zimetolewa kwa ajili ya waathirika.
Kwa mujibu wa Mtui, zoezi la upimaji viwanja katika eneo hilo lililotolewa na Jeshi la Magereza umefanyika kwa weledi na kukamilika ndani ya siku saba ambapo jumla ya viwanja 269 vilipimwa na kupandwa mawe
Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga ameishukuru Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kufanya kazi kubwa ya kupima viwanja na kuweka mawe katika kipindi cha muda mfupi.
Kwa upande wake Naibu Waziri Pinda amesema, wizara yake imeshafanya jukumu lake la msingi la kupima eneo hilo na kutoa wito kwa TARURA kuharakisha uchongaji barabara kuelekea eneo hilo ili kurahisisha usafirishaji vifaa.
Post Comment
No comments