Breaking News

LHRC, SHEIKH PONDA WATOA WITO KUACHIWA KWA MASHEIKH WALIO MAHABUSU KWA MAKOSA MBALIMBALI


Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Sheikh Ponda Issa Ponda  akiziungumza na waandishi wa habari (kulia kwake) Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga makao makuu ya kituo cha sheria na haki za binadamu jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga akifafanua jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya kituo cha sheria na haki za binadamu jijini Dar es salaam.
Bwana Ulatule mmoja wya ndugu wa Familia ya marehemu akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya kituo cha sheria na haki za binadamu jijini Dar es salaam.

Dar es salaam
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC) kimeiomba Tume ya Haki Jinai inayoendelea na zoezi la ukusanyaji maoni nchini kutumia fursa hiyo kutoa mapendekezo kwa Rais juu ya watuhumiwa wote wa makosa ya ugaidi waliokaa mahabusu kwa zaidi ya mwaka mmoja bila kesi kusikilizwa ili Mkurugenzi wa mashtaka DPP kuwaachia huru.

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amemtaka mwendesha mashtaka wa serikali awafutie mashtaka au awafikishe mahakamani kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Ombi hilo la LHRC kwa kushirikiana na Jumuiya na taasisi za Kiislam umekuja mara baada ya taarifa ya kifo cha Sheikh Saidi Mohammed Ulatule kilichotokea Machi 4 mwaka huu aliyekuwa akituhumiwa kwa ugaidi ambapo aliwekwa gerezani tangu mwaka 2016.

"LHRC tunashauri vifo vitokanavyo na watu kufia mahabusu vichunguzwe na tunatoa rai kwa serikali kupitia Ofisi ya Mwendesha Mashtaka kuwaachia huru watuhumiwa waliokaa zaidi ya mwaka mmoja mahabusu ama kuwapeleka mahakani ili wakahukumiwe" Alisema wakili Henga

Kwa upande wake Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Sheikh Ponda Issa Ponda pamoja na mmoja wa Familia ya marehemu Ulatule wameiomba serikali kufanya marekebisho ya sheria za vyombo vya dola pamoja na kutoa haki kwa mahabusu waliokaa muda mrefu gerezani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Machi 10 mwaka huu na Mkuu wa Magereza Dar es Salaam, George Wambura alisema kifo cha sheikh huyo kilichotokea Machi 4, mwaka huu, kimetokana na ugonjwa wa Moyo uliokuwa unamkabili tangu mwaka 2017 alipoingia gerezani.

No comments