CUF YATOA UFAFANUZI JUU YA UWEPO WA MAKUBALIANO YA KUMWACHIA RAIS SAMIA URAIS MWAKA 2025
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF- Chama Cha Wananchi)
CUF HAIHUSIKI NA MAKUBALIANO YA KUMWACHIA RAIS SAMIA URAIS MWAKA 2025
Chama kimepokea maswali mengi kutoka kwa wananchi wapenda Demokrasia ambao wamehoji juu ya msimamo wetu kama Chama kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025. Hilo limekuja kufuatia uvumi unaozagaa kwamba kuna vyama vimefanya makubaliano ya SIRI na Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr Samia Suluhu Hassan juu ya kumuachia agombee Urais bila kupingwa mwaka 2025.
Uvumi huo ulioanza chini chini mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu, unaonekana kuenea kwa kasi zaidi baada ya CHADEMA kumualika Rais Samia kuwahutumia Wanawake wa chama hicho kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8, mwaka huu ambapo Mheshimiwa Rais alitamka bayana kwamba ni matarajio yake kwamba CHADEMA hawana nia ya Kushinda Uchaguzi wa Urais mwaka 2025 na wanaCHADEMA wakashangilia kwa mayowe, makofi na vifijo huku wakiitikia "CCM OYEE".
Hali hiyo inayokosa tafsiri njema katika Siasa za Ushindani nchini imekolezwa na kauli ya hivi karibuni iliyotolewa na Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo kwamba mwaka 2025 watamwachia Dr SAMIA nafasi ya Urais na wao watasubiri 2030.
CUF- Chama Cha Wananchi ni magwiji na Walimu katika Maridhiano na Miafaka ya Kitaifa. Kwetu Maridhiano malengo yake ni kuandaa uwanja tambarare kwa ajili ya kufanya Siasa za Kiushindani katika mazingira ya Kistaarabu. Kamwe Maridhiano kwetu hayamaanishi kuiwachia CCM Ikulu, iwe kwa ahadi ya kupewa majimbo au kwa kupewa fedha za kufanyia mikutano nchi nzima.
Ni vema Wananchi pia wakajua tofauti iliyopo baina ya CUF- Chama Cha Wananchi na vyama vingine. Chama CHETU ni Chama Taasisi na Maazimio yake hufikiwa na vikao. Vipo vyama ambavyo viongozi wake Wakuu wanaweza kupitisha Maazimio na kuyatangaza HADHARANI wakiwa jukwaani bila kulazimika kufanya Kikao na hilo lisilete shida kwa wanachama wao kwa kuwa vyama hivyo si vya KITAASISI, ni vya watu binafsi.
Tunatoa wito kwa Watanzania wote waielewe dhamira ya dhati ya CUF- Chama Cha Wananchi katika ushiriki wake katika Maridhiano kwamba ni kwa lengo tu la kuhakikisha Demokrasia ya kweli inapatikana nchini, na si kwa kuiua kabisa Demokrasia kwa maslahi ya viongozi wa Vyama. Tuliposhiriki na kufanikisha Maridhiano na Muafaka wa Zanzibar wa mwaka 2009 uliozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), tulidhamiria kuleta Maendeleo na Ustawi kwa Wazanzibari bila ya kuangalia maslahi ya muda mfupi ya Chama au viongozi wake. Leo Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar inakihusu Chama chochote kitakachokidhi au kutangazwa kukidhi Masharti yake.
Hali kadhalika, Muafaka tunaoupigania kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais SAMIA ni kwa lengo la kufanikisha Maslahi Mapana ya Taifa hili.
Hivyo CUF- Chama Cha Wananchi hakihusiki na wala hakitohusika na makubaliano yoyote ya urafiki wa kuachiana Ikulu bila ya kushindania Ridhaa ya Wananchi.
Tunaamini kwamba CUF-Chama Cha Wananchi ndicho Chama pekee kilichobaki na dhamira ya kuing'oa CCM Madarakani 2025 wakati vyama vingine vikipitisha maamuzi ya kumwachia Ikulu Dr Samia Suluhu Hassan. Tunatoa wito kwa Wananchi wote wapenda mabadiliko na wanaochoshwa na tozo, kupanda kwa gharama za maisha kusikovumilika na adha nyingine tunazosababishiwa na Serikali ya CCM waache kushabikia vyama ambavyo tayari vimejitoa kwenye Mapambano ya Kuing'oa CCM MADARAKANI na badala yake tukusanye nguvu kupitia CUF- Chama Cha Wananchi ili tulete Mabadiliko ya Kimfumo na Kiutawala kwenye taifa letu.
CUF- Chama Cha Wananchi kinathamini mazuri mengi yanayofanywa na Rais Samia na Serikali yake, tunampongeza kwa hilo.
Hata hivyo, kama Chama Cha Upinzani, dhamira yetu ya kukamata Dola na kuiongoza nchi kwa Itikadi ya Utajirisho kwa Misingi ya Haki Sawa na Furaha kwa Wote haiwezi kuwekwa pembeni kwa sababu yoyote iwayo. Tunaomba mtuunge mkono.
HAKI SAWA NA FURAHA KWA WOTE!
Eng. Mohamed Ngulangwa
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma
CUF- Chama Cha Wananchi
Machi 15, 2023
No comments