Breaking News

WADAU WA NISHATI WAHAMASISHWA KUSHIRIKI MKUTANO NA MAONESHO YA PETROLI YA AFRIKA MASHARIKI

Dar es salaam:
Wadau mbalimbali katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia nchini wamehamasishwa kushiriki katika Mkutano na Maonesho ya 10 Petroli yanayotarajiwa kufanyika nchini Uganda mwezi Mei mwaka huu yatakayoshirikisha nchi zote za Afrika Mashariki.

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (aliyemwakilisha Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba) amewahamasisha wadau hao jijini Dar es Salaam katika Mkutano maalum uliolenga kuwafahamisha na kuwahamasisha ili waweze washiriki katika mkutano huo muhimu utakaofanyika Uganda kuanzia tarehe 09 hadi 11 Mei 2023. 

Byabato amesema, lengo la Mkutano huo wa Uganda ni kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia kwa kutangaza shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na Gesi Asilia zinazoendelea ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki ambapo Tanzania itapata fursa ya kueleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa mabomba ya Gesi Asilia na Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG).

“Mkutano na Maonesho hayo yataonesha watu mbalimbali wanafanya nini kwenye kuchimba, kutafuta, kwenye teknolojia, utoaji wa huduma na ni hatua gani ambayo nchi shiriki zimefika katika Sekta ya Mafuta na Gesi, hivyo leo tumewaelimisha na kuwafahamisha wadau wetu faida ya kushiriki katika Mkutano na Maonesho hayo.” Amesema Byabato

Kuhusu Gesi Asilia ameeleza kuwa Tanzania inafanya vizuri kwenye uchimbaji na uendelezaji wa Gesi Asilia kwani tayari inatumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo viwandani, majumbani na kuzalisha umeme ambapo asilimia 60 hadi 70 ya umeme unaozalishwa nchini unatokana na Gesi Asilia.

Ameongeza kuwa, Tanzania imejipanga kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya kupeleka Gesi nchini Kenya, Uganda na Zambia, hivyo itatumia Maonesho hayo pia kwa kutangaza soko la gesi nchini ili kupata wawekezaji zaidi si katika kuchimba tu, bali pia kuiendeleza Gesi Asilia.

Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Joyce Kisamo ameeleza kuwa, Tanzania itatumia fursa ya Maonesho hayo ya Uganda ili kuweza kujipanga vizuri na maandalizi ya Mkutano na Maonesho ya 11 ya Petroli ya Afrika Mashariki kwani Tanzania ndiyo itakuwa mwenyeji wa maonesho hayo.

Amesema Mkutano na Maonesho hayo yanasimamiwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki na yanazunguka katika nchi Wanachama na kuwa, Tanzania itakuwa mwenyeji wa Mkutano wa 11 ambapo itapata nafasi zaidi katika kuinadi Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia kwa kueleza fursa mbalimbali za uwekezaji, masuala ya kisheria, kanuni na miongozo.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia (ZPRA), Abdulkadir Juma amesema kuwa, Zanzibar imejipanga kushiriki katika Mkutano huo wa Petroli nchini Uganda kwani kuna maeneo ambayo yanahitaji uwekezaji katika Bahari Kuu hivyo watatumia fursa hiyo kujitangaza na kupata uzoefu kutoka kwa washiriki wengine.

Wadau waliohuria mkutano huo ni Taasisi za Elimu, Mabenki, Kampuni za Kimataifa za mafuta na Gesi asilia, Kampuni za Bima na Ukaguzi pamoja na Taasisi za Serikali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar zinazosimamia Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia.

Mkutano huo umeratibiwa na Wizara ya Nishati pamoja na taasisi zake za Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli, (PURA) Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na  Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA).





No comments