VIONGOZI WATAKIWA KUTAFSIRI MKATABA WA LISHE KWA WANANCHI
Na. Angela Msimbira - Dar es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Angellah Kairuki amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji na Vitongoji pamoja na wataalam wa Afya nchini kuhakikisha wanautafsiri Mkataba wa lishe kwa wananchi ili uweleweke
Ameyasema hayo leo Februari 23, 2023 Jijini Dar-es-salaam wakati alipowasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya kuanza ziara yake ya Kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye Majimbo ya Ukomga, Segerea na Kigamboni.
Amewataka viongozi hao kuhakikisha wanawashirikisha wataalam kwenye ngazi ya jamii ili waweze kuelewa kwa kina Mkataba huo na kuwa mabalozi wa kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa lishe nchini
Amewataka kuhakikisha kuwa mikutano inayofanyika kwenye ngazi ya Serikali za Mitaa suala la Mkataba wa lishe uwe ndio agenda kuu lengo likiwa kila mwananchi aweze kujua umuhimu wa lishe na kupunguza udumavu wa watoto nchini.
“Ni muhimu tukashuka hadi katika ngazi ya mitaa kuhakikisha tunatoa elimu ya kutosha kuhusu Mkataba wa lishe, kwa kufanya hivyo kutasaidia kila mmoja kujua umuhimu wa lishe nchini” amesisitiza Waziri Kairuki.
Waziri Kairuki amewaagiza viongozi hao kuhakikisha Mkataba wa Lishe unajulikana na kueleweka kwa wananchi ili kuweza kujua hali ya uduni wa lishe, udumavu lengo likiwa ni kupima utekelezaji wa mkataba huo
Aidha ameupongeza Mkoa wa Dar-es-salaam kwa kutekeleza Mkataba wa lishe kwa asilimia 95 lakini amewataka kuhakikisha wanautafsiri mkataba huo kwa wananchi ili uweze kueleweka na kupata matokeo yanayotegemewa na Serikali.
Vilevile Waziri Kairuki amewaagiza viongozi hao kuhakikisha wanafanya utafiti wa kina kuhusu mawakala wanaopatiwa POS kwa ajili ya kukusanya mapato kwenye Halmashauri kwa kuwa wengi wao huzizima na kutozisajili na hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa mapato
Amewataka kuongeza usimamizi na kujiridhisha kwenye upatikanaji wa Mawakala wanaoteuliwa kwa ajili ya kukusanya mapato ya Halmashauri pamoja na kuangalia kamisheni zinazotolewa kama ni kiwango sahihi na ndicho kinachotakiwa
Aidha, amewaagiza viongozi hao kuhakikisha kunakuwepo na uwazi katika kuwapata Mawakala wa ukusanyaji wa Mapato na kuweka mifumo ambayo itapunguza mianya ya upotevu wa mapato kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa
No comments