MHE. MCHENGERWA AANZIQL WAWA, AZINDUA MAGARI 22 YA DORIA, ASISITIZA UHIFADHI NA KUJITANGAZA
Na Mwandishi wetu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mohamed Mchengerwa leo ameyazindua magari 22 maalum kwa ajili ya kuimarisha shughuli za doria katika vituo 22 vya Mapori ya Akiba na Tengefu na Vituo vya Kudhibiti Wanyamapori wakali na waharibifu.
Aidha, amesema pia magari hayo yatumike kujenga mahusiano mazuri na wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi ili kupata taarifa za uhifadhi wa raslimali.
Uzinduzi huo umefanyika kwenye Ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).
Tukio hili ni la Kwanza mara baada ya kuteuliwa kuongoza Wizara hii na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yeye na Dkt. Hassan Abbasi ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara hii.
Waziri Mchengerwa amefafanua kuwa magari haya ni nyenzo muhimu katika kuwawezesha makamanda na askari kufika katika maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kuimarisha shughuli za doria za kudhibiti ujangili na wanyamapori wakali na waharibifu.
Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumwamini na kumteua kuiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii na kutoa magari haya ambapo amewataka kuyatunza ili dhamira ya Mhe.Rais ya kutaka kuboresha uhifadhi na kutangaza vivutio vya Utalii ifikiwe.
Amemwahidi Mhe. Rais kuendelea kufanya kazi kwa weledi na ubunifu ambapo ametoa kwa watendaji.
Aidha, amemshukuru Mhe. Rais kwa kutoa kipaombele katika sekta hii kwa kuitangaza Tanzania na vivutio vyake kwa kutengeneza filamu ya Royal Tour.
Amefafanua kuwa katika kipindi hiki kila mtendaji wa Wizara anatakiwa kubadilika na kufanya kazi zaidi ili kuongeza mchango wa sekta hii katika pato la Taifa.
Ameongeza kuwa kazi kubwa ni kuhifadhi na kutangaza ambapo ametoa siku tatu kupata taarifa ya taasisi zote chini ya Wizara hiyo.
Amewataka watendaji wabadilike, na wafanye maamuzi badala ya kusubiri na mambo yaharibike.
Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Fatma Mwasi kupitia kwa Waziri Mchengerwa ameiomba Serikali kutafakari lengo la kuwataka watumishi wa TAWA kuhamia Dodoma ambapo amesisitiza kuwa kuhamia huko kutadhoofisha uhifadhi wa raslimali za taifa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TAWA, Maj. Gen (Mstaafu) Hamis Semfuko amemhakikishia, Mhe. Waziri kuendelea kufanya kazi kwa weledi zaidi kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.
Katika ziara hiyo Mhe.Mchengerwa ameambatana na Naibu Waziri, Mhe. Mary Masanja, Katibu Mkuu, Dkt. Hassan Abbasi na Naibu Katibu Mkuu Juma Mkomi.
No comments