Breaking News

DKT. MPANGO ATAKA USHIRIKIANO WA PAMOJA KUMALIZA VIFO VYA WATOTO VITOKANAVYO NA UGONJWA WA UKIMWI

Dar es salaam:
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amesema ni muhimu kuwepo ujumuishi pamoja na ushirikishwaji wa sekta mbalimbali pamoja na jamii katika kukabiliana na changamoto zinazokwamisha ustawi wa watoto na wanawake.

Amesema hayo leo tarehe 1 Februari 2023 wakati akizindua Mkakati wa Kidunia kwa Kanda ya Afrika wa kutokomeza Ukimwi kwa Watoto ifikapo mwaka 2030, katika mkutano unaofanyika katika kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) Dar es salaam.

Amesema nchi zote kwa pamoja ni lazima kutambua vema jukumu lake ili kufikia lengo la kukomesha Ukimwi kwa Watoto ifikapo 2030 ikiwa ni pamoja na kushirikisha sekta binafsi katika azma hiyo muhimu.

Amesema ili kufanya Muungano huo wa kutokomeza Ukimwi kwa Watoto kuwa wa maana, halisia na wenye mafanikio ni lazima nchi za Afrika kuendelea kuchukua hatua za makusudi kuweka sera na mikakati muhimu, kujenga uwezo na kuendelea kufuatilia na kutathmini maendeleo ya hatua mbalimbali za mapambano hayo. ameongeza kwamba ni muhimu kujitolea kamili kwa nia na kusudi pamoja na kuwa na mipango ya kuwalinda watoto, wanawake na vijana dhidi ya matukio ya hatari na yasiyo ya lazima kama vile ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia na mila zote zinazowaweka hatarini ikiwemo ukeketaji.

 Makamu wa Rais Dkt. Mpango amesema Serikali ya Tanzania imedhamiria kukomesha janga la Ukimwi kama tishio kwa afya ya jamii ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni sehemu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu. Amesema Kufikia Septemba 2022, asilima 92 ya watu walijua hali yao ya maambukizi huku asilimia 98.3 wakiwekwa katika mpango wa matumizi ya dawa za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVs). 

Aidha amesema Serikali ya Awamu ya 6 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Global Fund, PEPFAR na sekta binafsi inaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika maabara za VVU za utunzaji na upimaji wa kawaida ambapo katika kipindi cha miaka miwili imefanikiwa kutoka katika maabara 54 hadi Maabara 130.



No comments