ITRACOM YAJIPANGA KUTATUA KERO YA MBOLEA NCHINI
Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha mbolea Itracom, Nduwimana Nazaire (katikati) akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari walipotembelea eneo la uzalishaji kueleza kazi inayofanywa na mitambo iliyopo eneo hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha mbolea Itracom, Nduwimana Nazaire akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea kiwanda hicho kilichopo Nala Jijini Dodoma leo tarehe 11 Januari, 2023.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo akizungumza na wahariri wa habari nchini waliotembelea kiwanda cha mbolea cha Itracom Nala Jijini Dodoma tarehe 11 Januari, 2023
Dodoma:
Imeelezwa kuwa ifikapo 2030 hakutakuwa na uingizaji wa mbolea kutoka nje ya nchi kufuatia uwezo wa viwanda vya ndani kuzalisha kiasi kinachotosheleza mahitaji ya nchi.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 11 Januari, 2023 na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo wakati wa ziara ya wahariri wa vyombo vya habari nchini katika kiwanda cha kuzalisha mbolea cha Itracom kilichopo Nala Jijini Dodoma.
Dkt. Ngailo amesema ujenzi wa viwanda vya mbolea ni utekelezaji wa sera inayotokana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kuhakikisha ifikapo 2025 uzalishaji wa mbolea nchini unafikia tani 800,000.
Akieleza kuhusu mbolea zilizosajiliwa nchini mpaka sasa, Dkt. Ngailo alisema aina 420 za mbolea zimesajiliwa na zinakidhi viwango vinavyotakiwa nchini.
Aidha, Dkt. Ngailo amesema, Mwekezaji wa kiwanda cha Itracom atazalisha mbolea kulingana na mahitaji ya mlaji baada ya kupima afya ya udongo na kubaini aina ya virutubisho vinavyopungua kwenye shamba lake.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Itracom, Nduwimana Nazaire amesema, awali mwekezaji alijipanga kuzalisha tani laki sita lakini kufuatia mahitaji makubwa ya mbolea nchini atazalisha tani milioni moja kwa mwaka.
Nduwimana amesema, kiwanda hicho kimejikita katika kuzalisha mbolea za asili (organal mineral fertilizer) zinazofanya vizuri kwenye uzalishaji na kimejengwa kwa muda wa mwaka mmoja na miezi mitano mpaka kilipoanza uzalishaji wa awali.
No comments