Breaking News

TALGWU YAJIVUNIA MAFANIKIO KATIKA KIPINDI CHA JANUARI HADI JUNI 2022

CHAMA cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kimeiomba Serikali kuipitia na  kufanya mabadiliko sheria ya tozo za miamala ya kibenki kuepuka makato ya mara mbili katika mishahara ya mtumishi wa umma. 

Akizungumza Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Chama kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2022, Mkuu wa Idara ya Habari na Uhusiano wa (TALGWU) bi Shani Kibwasali amesema tozo hizo tangu kuanza kwake zimekuwa zikizidi kumbebesha mzigo mfanyakazi ikizingatiwa mishahara wanayopata haikidhi mahitaji ya kila Siku na familia zao.

“Pia naomba nizungumzie suala la tozo za kibenki lililoanza kutekelezwa hivi karibuni. Tozo hizi zinawaathiri sana wanachama Wetu. Ikumbukwe kwamba watumishi wa umma kila mwezi wanalipa Kodi kwa kukatwa katika mishahara yao,” Alisema Bi. Kibwasali,

Alisema tangu kuanza kutekelezwaji wa sheria hiyo ya tozo ya miamala ya kutoa na kuhamisha fedha katika benki inamfanya mtumishi wa umma kutozwa zaidi ya mara mbili katika Pato moja kwa mwezi.

Bi Kibwasali aliongeza kuwa suala la nyongeza ya mishahara ni ukweli usiofichika kuwq bado wanachama wao ni wahanga wakubwa kwani bado yapo manung’uniko na TALGWU kama msemaji wao hawajaridhika kabisa kwa jinsi nyongeza ya mshahara ilivyofanyika.

“Napenda kuvhukua nafqsi hii niwatoe hofu wanachama wetu suala hili linashughulikiwa na Chama kwa kushirikiana na shirikisho la vyama huru vya Wafanyakazi nchini (TUCTA),” Alibainisha Bi. Kibwasali.

Akizungumzia mafanikio ya chama hicho katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Juni mwaka huu, , Bi Kibwasali amesema hadi kufikia Juni 2022 kulikuwa na jumla ya kesi 140 ambapo mawakili wa Chama wanasimamia kesi 100, mawakili wa nje wanasimamia kesi 13, na rufaa zilizopo Tume ya Utumishi wa Umma ni 27.

Alisema Chama kiliandaa utetezi kwa watumishi 12 waliokuwa wamepewa mashataka na waajiri. Hivyo kati ya kesi 140 zilizoisha ni 39 na chama kimeshinda ya kesi 35 na kushindwa kesi nne huku kesi nyingine zikiendelea Mahakamani.

Bi. Kibwasali aliongeza kuwa katika kipindi hicho TALGWU kilikuwa na jukumu jingine kubwa la kushughulikia haki na stahiki za wanachama ambazo kimsingi zipo kwa mujibu wa sheria ya Utumishi wa Umma na kanuni zake.

"Chama kinajivunia kuona Serikali imetekeleza maombi yao katika maeneo ya kama upandishaji vyeo, mishahara, malipo ya malimbikizo ya mishahara na utawala Bora" Alisema Bi Kibwasali.
 

No comments