Breaking News

WAZIRI PROF NDALICHAKO ARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MFUKO WA FAIDIA KWA WAFANYAKAZI (WCF)

Profesa Ndalichako alibainisha hayo jana mkoani Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Menejimenti, Wafanyakazi na Bodi ya mfuko huo ampapo aliupongeza uongozi wa WCF kwa kazi nzuri wanayofanya.

”Nimeridhishwa na namna mlivyojipanga kuwahudumia wafanyakazi waliopata changamoto wakiwa kazini,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema mfuko huo ni muhimu kwa wafanyakazi kwani unaonyesha namna wanavyothaminiwa wanapopata changamoto.

Waziri huyo alibainisha kwamba kuanzia 2015 Sheria ya mfuko huo ndiyo ilianza kufanya kazi na ndani ya miaka sita mfuko umesajili waajiri 28,152 huku walioanza kuutumia ni 26,080.

Vile vile Waziri Ndalichako aliupongeza mfuko huo kwa zaidi ya asilimia 85 kufanya shughuli zake kwa njia ya Tehama.

Alitoa wito kwa wafanyakazi wanapopata matatizo wahakikishe wanawasilisha nyaraka zao mapema ili waweze kuhudumiwa kwa wakati ikiwemo malipo na huduma za matibabu.

Waziri Ndalichako aliahidi kuwa atahakikisha watomishi wanaopata changamoto kazini wanapata haki yao kwa wakati.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Patrobasi Katambi alisema ni muhimu kwa waajiri kujiunga na mfuko huo ili wafanyakazi wao wanapopata changamoto za kiafya uweze kuwasaidia.

“Lakini pia wafanyakazi kama hawajaingizwa kwenye mifuko ya namna hii waweze kutoa taarifa, kwani ni kwa faida yao,” alisema Katambi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya WCF Emmanuel Umbo alisema kuwa pamoja na kwamba mfuko huo ni mchanga, lakini umejidhatiti kuliko mifuko mingine.

Hata hivyo alisema kuwa mfuko huo una ofisi tisa tu nchi nzima, hivyo alimuomba Waziri Ndalichako kuusaidia kuwa na ofisi nchi nzima hata kama zitakuwa ndigo ili uweze kuhudumia wafanyakazi wote kwa ufanisi na kwa wakati.

“Tunaomba utuwezeshe kila Mkoa uwe na ofisi hii, hata kama ni ndogo ili kusaidia wafanyakazi. Nisisitize tunaomba huu mfuko ufike kila Mkoa na ofisi yako tunaomba itusaidie,” alisema Umbo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa WCF John Mduma alimuahidi Waziri Ndalichako kwamba watatekeleza maagizo yake ikiwemo kuweka misingi bora ya Tehama ili kuhakikisha huduma zinakuwa bora.

 

No comments