Breaking News

MAIMUNA SAID APITISHWA NA CHAMA CHA ADC KUGOMBEA NAFASI YA USPIKA WA BUNGE.. HAMAD RASHID AMPA WOSIA


Chama Cha Alliance For Democratic Change kimempitisha rasmi Maimuna Said Kassim kuwa Mgombea nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutoa wito kwa wabunge kumpa kura za ndio bila kujali itikadi za kisiasa.

Akizungumza makao makuu ya chama hicho Buguruni Jijini Dar es salaam, Mwenyekiti Taifa wa ADC mhe. Hamad Rashid Mohamed amesema chama kimempitisha Bi. Maimuna mara baada ya kamati tendaji ya Chama kujiridhisha kuwa anao uwezo, elimu ya kutosha pamoja na weledi mkubwa hivyo anaweza kuwaongoza wabunge kama kiongozi mkuu wa Mhimili huo.

Alisema katika kipindi kirefu kumekuwepo na kasumba kuwa spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hasa wabunge wa chama tawala kumchagua Spika anaetokana na chama chao bila kujali uwezo wake,hali ambayo inachangia kuleta migongano yakimihimili katika nchi.

"Hatuna mashaka na uwezo wa Maimuna Said kwani hata katika uchaguzi mkuu uliopita aligombea ubunge katika jimbo la kilindi na alipata zaidi ya kura elfu kumi na nane, hivyo anao uwezo wa kuliongoza bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania" Alisema Mhe.Rashid

Alisema Chama cha ADC hakipeleki mgombea kwa kutafuta CV kama inavyozungumzwa huko nje bali Chama kina amini katika misingi ya kutengeneza Viongozi hii ndio moja ya sifa ya chama na si vinginevyo.

"Chama cha ADC kimekuwa tanuru la kupika na kuandaa viongozi wenye uwezo na kiaminika hivyo kuteuliwa katika nafasi za uongozi ndani ya serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Queen Sendiga na sasa tunakwenda kutoa kiongozi mwingine ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania". Aliongeza mhe. Hamad

Katika hatua nyingine mhe hamad amempongeza rais Samia kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya tangu alipoingia madarakani kuwaunganisha na kuwaletea maendeleo watanzania katika kipindi kifupi alichohudumu chama cha ADC kitaendelea kumuunga mkono na kumpa ushirikiano wa karibu kuweza kufikia malengo.
Kwa upande wake mgombea wa kiti cha Uspika, Bi Maimuna Said Kassim akizungumza mara baada ya kutangazwa kupitishwa na chama hicho kuwa mgombea amewashukuru Viongozi wa Chama chake kwa kumwamini na kumuona anafaa kupeperusha bendera ya cha hicho katika uchaguzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Nilijitathimini nikaona nina uwezo, nina elimu ya kutosha na uzoefu katika Uongozi katika maeneo mbalimbali ikiwepo Chuo kikuu cha Dodoma, Nimesoma masuala ya Siasa na Uongozi hivyo nina hakika kama wabunge watanichagua nitafanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa" Alisema Bi. Maimuna.

Alisema ninayo dhamira dhabiti ya kuleta mageuzi chanja kwa kulifanya bunge kuwa la kisasa kwani katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na migongano ya kimihili endapo watanipa ridhaa nitahakikisha na kulirudisha heshima yake kwa kulifanya bunge kuwa imara zaidi"

Aidha Bi. Maimuna ameongeza kuwa anaimani kubwa atakwenda kupata kura za ndio na watanzania wategemee mabadiliko makubwa yanakwenda kutokea katika kipindi changu cha uongozi.

No comments