Breaking News

FILAMU YA BINTI YAIPEPERUSHA BENDERA YA TANZANIA DUNIANI


Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mwandishi na Muongozaji wa Filamu hiyo Bi. Seko Shamte alisema Filamu yake tayari imeshaanza kuonekana katika jukwaa la Netflix kuanzia Tarehe 07 Januari, 2022.

“tumepata nafasi ya kuoneshwa Duniani kote, kuna kazi zingine kutoka Afrika hazionekani nje ya Afrika, lakini Filamu yetu imepata bahati ya kuonekana kila pembe ya Dunia bila kikwazo chochote” alisema Bi. Seko Shamte.

Alieleza kuwa, Filamu hiyo imetayarishwa na Wanawake, kuanzia Uandishi wa mswada, Uigizaji, Uongozaji na Uhariri, hivyo mafanikio ya kazi hiyo ni ishara ya ukuaji wa uwezo wa Wanatasnia Wakike nchini.

Bi. Seko Shamte aliishukuru Serikali kwa kumuunga mkono katika mafanikio ya Filamu yake tangu hatua ya Utayarishaji hadi sasa kuonekana Netflix. Aidha, alimalizia kwa kutanabaisha kuwa, mafanikio ya Filamu hiyo yanaenda sambamba na kuitangaza Nchi Kimataifa.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo aliwapongeza Watayarishaji kwa hatua hiyo kwakuwa ni kwa mara ya kwanza Filamu kutoka Tanzania kuoneshwa katika jukwaa hilo, ambapo ni nchi Tatu pekee kutoka Afrika zimeshapeleka Filamu zao, ambazo ni Kenya, Nigeria na Afrika Kusini, ila kwasababu ya ubora, Filamu yetu imefanikiwa kwenda huko.

Dkt. Kilonzo alieleza kuwa, mafanikio hayo ni mapinduzi kwenye Tasnia ya Filamu nchini, kwani imepiga hatua kubwa katika eneo la Usambazaji, ambapo sasa inasambazwa kupitia jukwaa kubwa linalotazamwa na Watazamaji zaidi ya milioni 200 Duniani.
Kwa upande wake Raisi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Bw. Eliya Mjatta alitoa rai kwa Wadau wa Filamu na Watanzania kwa ujumla kuiunga mkono Filamu hiyo kwa kuitazama katika Jukwaa la Netflix ili kuonesha tija ya kazi hiyo katika Mtandao huo.

Naye Mshindi wa Tuzo ya Muigizaji Bora kupitia Tuzo za Filamu Tanzania 2021, Bi. Godliver Gordian alimalizia kwa kuwashauri Watayarishaji kutayarisha Filamu zenye uhalisia wa Maisha ya Jamii zetu kama ilivyo Filamu ya Binti, na ndio maana imefanikiwa kufika mbali.
Filamu hiyo imefanikiwa kuoneshwa kwenye matamasha makubwa ya Filamu katika nchi za Marekani, Ujerumani, Nigeria, Afrika Kusini na New Zeland.


No comments