Breaking News

WAZIRI JAFO : MABADILIKO YA TABIA NCHI NI AGENDA KUU KWA SASA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo amesema suala la Mabadiliko ya Tabianchi lipo na madhara yake yanaonekana katika sehemu mbalimbali kwenye nchi yetu ya Tanzania.

Ameyasema hayo leo Novemba 14, 2021 wakati wa mbio za kuhamasisha utunzaji wa mazingira (MAZINGIRA MARATHON) zilizofanyika kwenye viwanja vya Green Oysterbay Jijini Dar es Salaam. Mbio hizo zililenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
Mhe. Jafo amesema dunia kwa sasa ipo hatarini kutokana na mabadiliko ya Tabianchi na kuna baadhi ya maeneo yamesha athiriwa na athari za mabadiliko hayo kama kutoweka kwa Kisiwa cha Kifungu.

Mhe. Jafo ameongeza kuwa kina cha maji kinazidi kuongezeka mfano kwenye visiwa vya Pemba hali inayopelekea uwekezaji kupungua na baadhi ya makazi ya watu hayatakuwepo tena.
Kwa upande wa maziwa Tanganyika na Ziwa Viktoria vina vya maji pia vimeongezeka jambo ambalo linapelekea kuharibika kwa miundombinu na kupoteza uwekezaji uliokuwa karibu na fukwe za maziwa haya.

Aidha Mhe. Jafo ametoa wito kwa Watanzania kuwa na desturi ya kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
Nae Meneja wa Kanda ya  Mashariki Kaskazini NEMC Bw. Anorld Mapinduzi amesema ushiriki wa NEMC kwenye mbio hizo ni sehemu ya kuhamasisha utunzaji wa mazingira sambamba na kufanya mazoezi kwa kuweka afya ya mwili vizuri.

"Tunapozungumzia mazingira tuna maanisha Afya na mazingira endelevu,  mambo haya mawili huwezi kuyatenganisha. Huwezi kuwa na afya nzuri kama hutunzi mazingira unayoishi, mfano  ikiwa utakata miti huwezi kupata hewa safi na salama na afya itakuwa hatarini".
Bw. Mapinduzi amesisitiza zaidi suala la upandaji miti ili izalishe hewa hewa ya Oksijeni ambayo ni muhimu katika mfumo wa upumuaji, vile vile miti inasaidia kufyonza hewa ya ukaa ambayo inazalishwa na viwanda vyetu
Kwa upande wake mratibu wa mbio hizo Mazingira Marathon bw. Amon Mkonga amesema lengo kibwa la kuandaa mbio hizo pamoja na washirki kufanya mazoezi pia ni kuunga mkono juhudi za rais Samia ya kuhakikisha utunzaji wa mazingira.

"Pomoja na washiriki kufanya mazoezi mbio hizi pia ni moja ya hatua ya kuunga mkono juhudi za mhe rais Samia za kuhakikisha elimu inatolewa kwa jamii ya kutambua faida na umuhimu wa uhifadhi wa mazingira"


 

No comments