Breaking News

AFRICAN COURT YAWAPIGA MSASA WANAHABARI JIJINI DAR

MAHAKAMA ya Afrika ya Haki za Binadamu  na Watu (African Court) inafanya kazi na Umoja wa Afrika (UA) kuimarisha utekelezaji wa maamuzi ya kesi kwa vile maamuzi mengi ya kesi zake hayatekelezwi kikamilifu.

Kulingana na msajili wa mahakama hiyo, Dkt. Robert Ewo, katika maamuzi 120 ambayo yametolewa na mahakama hiyo tangu kuanzishwa kwake, ni chini ya asilimia 10 pekee ndiyo yametekelezwa kikamilifu.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu ya wanahabari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 28,2021, Dkt Ewo alisema hali hiyo inaleta changamoto kubwa kwa mahakama hiyo.

"Katika kipindi cha miaka 15, mahakama imepata mafanikio makubwa.Tumepokea zaidi ya kesi 330 zimepokelewa na mahakama imetoa maamuzi ya kesi zaidi ya 120, lakini changamoto ipo katika utekelezaji wa maamuzi ya nchi wanachama.... hii inakatisha tamaa sana". Amesema 

Amesema mahakama ipo kusaidia nchi za Afrika kutimiza ahadi zao kuhusu haki za binadamu.

Amesema mahakama imefanya maamuzi juu ya haki ya uhuru wa kujieleza, haki ya watu wa kiasili na haki ya serikali shiriki miongoni mwa mengine, ambayo yanasaidia kuimarisha hali ya kijamii na kiuchumi na kisiasa ya nchi.

“Kuhusu suala la utekelezaji wa maamuzi ya mahakama hii ni changamoto kubwa inayoikabili mahakama, inakatisha tamaa sana, hivyo tunashirikiana na AU na nchi wanachama kuhakikisha maamuzi hayo yanatekelezwa.” Amesema.

Msajili huyo ameongeza; "Kuna mkutano mwezi ujao ambao utaleta pamoja nchi wanachama na huko, tutajadili kwa kina ni changamoto zipi ambazo Mataifa yanakabiliana nayo na kushindwa kutekeleza maamuzi ya mahakama."Amesema

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Jaji Tujilane Chizumila, jaji wa AfCHPR amesema vyombo vya habari vinafanya kazi muhimu ya kuelimisha umma juu ya haki za binadamu.

Mafunzo hayo yamewakutanisha waandishi wa habari zaidi ya 20 kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika ili kuwaelimisha na kuwawezesha kwa ujuzi muhimu zaidi ili kuimarisha utoaji wa taarifa za haki za binadamu na haki.

Mafunzo hayo pia yataviwezesha vyombo vya habari kutoa elimu kwa nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika juu ya umuhimu wa mahakama na kuwahimiza kutumia uwepo wake.

Jaji Chizumila ambaye amezungumza kwa niaba ya Rais wa AfCHPR, Jaji Iman Aboud, amesema vyombo vya habari vinafanya kazi muhimu ya kuelimisha umma juu ya haki za binadamu.

Amesema ili vyombo vya habari vitekeleze vyema jukumu lao la waangalizi wa utawala wa haki za binadamu, vinapaswa kufundishwa kushughulikia eneo maalum na la kipekee la haki za binadamu, mipaka yake, uamuzi, utekelezaji na athari.

Amesema: "Kutokana na mazingatio haya, mawasiliano kuhusu mahakama yanapaswa kuandaliwa ili kukidhi mahitaji ya wadau wake mbalimbali na kuwapa uwezo kwa kila mmoja kutekeleza wajibu wake ipasavyo katika mlolongo wa matendo yake."

"Mahakama za Afrika zitaendelea kufanya kazi kwa karibu na kujenga uhusiano na vyombo vya habari nchini na nchi zote Wanachama. Vyombo vya habari vinapaswa kuendelea kuwa wabunifu, kutumia teknolojia ili kuwa na ushindani" alisema.

Chombo cha mahakama cha Umoja wa Afrika kinaundwa na nchi wanachama 55 zenye wafanyakazi 70 kutoka mataifa yote ya Kaskazini, Magharibi, Kusini, Mashariki na Kati.

Mahakama hiyo pia inatekeleza mipango kadhaa ya kuimarisha programu za uhamasishaji na kuelimisha Mataifa ya Afrika juu ya umuhimu wa nchi.
Baadhi ya wadau wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu  na Watu (African Court) waliohudhuria mkutano unaofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya wadau wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu  na Watu (African Court) wakiwa ktk picha ya pamoja jijini Dar es Salaam.

No comments