Breaking News

TANZANIA, AFASU Wasaini Makubaliano ya Ushirikiano Kuwezesha na Kukuza Uwekezaji, Biashara na Utalii Nchini

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Geoffrey Mwambe Pamoja na Raisi wa Jumuiya ya Muungano Kimataifa chini ya kundi la Afrika na Asia (Afro- Asian union (AFASU) Dr. Hossam Darwish wametia saini hati ya makubaliano ya  Ushirikiano kuwezesha kukuza  na kuunda ushirikiano katika sekta ya uwekezaji , wenye lengo la  kuwezesha na kukuza uwekezaji, biashara na utalii nchini Tanzania . 

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo iliyofanyika katika Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu Jijini Dar es salaam, Mhe. Mwambe ameainisha maeneo ambayo Tanzania na ASAFU watashirikiana katika kuvutia maeneo ya uwekezaji kuwa ni pamoja na uwekezaji katika Afya,kilimo, Viwanda, Biashara Mtandao, Utalii, Elimu pamoja na Uwekezaji katika TEHAMA.

Mhe. Mwambe ameeleza kuwa kusainiwa kwa hati ya makubaliano kunaonyesha dhamira kubwa ya serikali ya awamu ya sita  ya kushirikiana na wadau wote  duniani  na kuwaalika katika uwekezaji lakini pia kutumia fursa  ya kuaminika kama  serikali ya Tanzania  kuweza kuwaomba  Taasisi  na sekta binafsi waweze kutusemea  ili kushawishiana kuja kuwekeza Tanzania kwasababu ya mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa nchini.

“Serikali ya awamu ya sita inaaminika  na mazingira ya uwekezaji Tanzania yameendelea kuboreshwa  na pia sisi  kwenye Nyanja za kimataifa  tafsiri yake ni kuwa tanzania inaendelea  kusifika kwenye  ubora wake wa mazingira ya uwekezaji”Amesema Mhe. Mwambe

Aidha Mwambe amewashukuru wawekezaji hao na kuwahakikishia kuwa ofisi yake iko tayari kushirikiana nao kwa kuweka mazingira wezeshi ili kuhakikisha wanafanikiwa, na kuwataka watanzania na Taasisi nyingine za serikali  kuwapa ushirikiano wa kutosha ili waweze kufanikiwa kuwekeza nchini. 

“Nawashukuru sana AFASU, nawakaribisha sana na ninawaomba watanzania tuendelee kuwapa ushirikiano wote  pale ambapo wataitaji vibali, ardhi,  na idhini mbalimbali za serikali  ili waweze kutekeleza mradi wao  tutahakikisha kwamba tunasimamia hilo  kwahiyo tusingependa kuwakwamisha  kwa sababu hii inatupa sifa sisi na  inampa pia amani Mhe. Rais na kuendelea kujenga imani kubwa kwa  wawekezaji wa ndani na nje ya nchi

Kwa upande wake Rais wa Jumuiya hiyo, Dkt. Hossam Darwish amesema Jumuiya ya AFASU wako tayari kutekeleza vipengele vyote ambavyo  vimo ndani ya makubaliano  hayo na watatekeleza kwa nguvu kubwa na  haswa kwa kuanza na sekta ya kilimo  ambapo ndani ya Jumuiya   wanao wajumbe ambao  ni  wawekezaji wakubwa kwenye sekta ya kilimo   ambapo wameona maeneo ya kilimo na  wamevutiwa sana na fursa  hiyo ya kilimo hapa nchini  na hivyo  wanatoa ishara njema  kwamba wao watakuwa ni sehemu ya uwekezaji katika sekta hii ya kilimo  pamoja na sekta nyingine ambazo zitakuwa zimeainishwa katika makubaliano. 

Dkt. Hossam ameongeza kuwa  kwa hatua ya kwanza na kwa haraka wataanza na mradi  wa chuo  cha  Kimataifa cha Kitanzania  cha mifumo ya kielektroniki ambacho kitakuwa na vitivo vitivo 14 vya kimasomo  ya kielimu na wanaimani kwamba vitivo hivyo  vinaweza kwenda sambamba  na kile walichokiona kinahitajika ndani ya nchi yetu   ambapo shahada mbalimbali zitatolewa kupitia chuo hicho na kitaweza kuchukua wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali za Afrika na nje ya Afrika, nakuhakikisha kuwa mfumo wa masomo utaweza kutoa wataalamu wa kutosha.

Amesema hatua nyingine itakayofuata ni mradi wa maonyesho ya biashara ambayo yatafanyika hapa nchini Tanzania ili kuweza kuchochea uwekezaji na pia jumuiya hiyo itajikita katika uwekezaji wa masuala ya utalii hususan katika ujenzi wa hoteli zenye hadhi kubwa na katika sekta ya afya watajikita katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha Dawa na vifaa Tiba .

Kwa upande mwingine Dkt. Hossam amemshukuru Waziri wa Uwekezaji kwa  kuonesha uzalendo mkubwa kwa nchi yake ambapo amekuwa na juhudi kubwa sana  na kwa upande wake anamatumaini makubwa kuwa Tanzania itapiga hatua katika sekta hii ya uwekezaji kwa juhudi kubwa ambazo anazifanya Waziri wa Uwekezaji.

Hafla hiyo ya utiaji Saini wa hati ya makubaliano ya Ushirikiano ilihudhuriwa na Mkurugenzi  Mtendaji wa kituo cha Uwekezaji Tanzania, Dkt. Maduhu Kazi, na Mkurugenzi Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Latifa Khamis, pamoja  na maafisa wa serikali kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Misri, Wizara ya mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
 

No comments