RC Sophia Mjema Awataka Viongozi Ngazi za Mtaa na Vijiji Kuwajibika kwa Wananchi
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Edward Mjema amewataka viongozi wa serikali kuanzia ngazi za mitaa na vijiji kuwajibika kwa kusikiliza kero za wananchi ili kuleta maendeleo.
Mhe. Mjema ameyasema hayo leo Jumanne Oktoba 12,2021 wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi baina yake na aliyekuwa Mkuu wa mkoa huo Dkt. Philemon Sengati.
"Ninataka Super Sonic Speed katika kuleta maendeleo kwenye mkoa wa Shinyanga.Ili kufikia maendeleo ni lazima kila mmoja awajibike. Nataka kuona vibe, nataka kuona mtetemeko wa Shinyanga", amesema RC Mjema.
"Viongozi kuanzia ngazi za mitaa tatueni matatizo ya wananchi, msikwepe majukumu yenu kwa kuogopa kuwa mtaonekana wabaya, msikae ofisini, lazima tukawatumikie wananchi..siku ya kupumzika ni siku ambayo utakuwa kwenye likizo yako, nenda kwa wananchi na tutapimana na kuulizana umefanya nini.... Lazima tuwe serious kuonesha kuwa Shinyanga inaendelea", amesema Mjema.
Amewataka viongozi kutokuwa sehemu ya migogoro katika jamii huku akiwataka viongozi kutatua matatizo ya wananchi badala ya kusubiri viongozi wa ngazi za juu waje.
Mjema amesisitiza kuwa atakuwa mkali kwa viongozi watakaotumia hovyo fedha za serikali na kwamba mtumishi wa serikali lazima awe mfano kwa wananchi kwa kuepuka mambo ya hovyo mtaani.
"Kiongozi wa serikali lazima uwe smart, uwe na nidhamu, kaa na nidhamu watu wakuone wewe ni kiongozi mwenye nidhamu. Tuwe na nidhamu, tuwajibike na tuwe mfano mzuri kwa wananchi..Ukiona pagumu nenda katafute pengine, Madam ushakuwa kiongozi wa serikali lazima uwe na nidhamu", amesema Mjema.
"Mhe. Rais Samia pia ametusisitiza kuachana na vitendo vya rushwa...Huku kwenye rushwa ndiko kwenye matatizo mengi, huku tutafanya kazi kubwa, kasafisheni nyumba zenu ili tuhakikishe kila tunapopita pako safi", ameongeza.
Mkuu huyo wa mkoa pia amesema hatapenda kuona mimba na ndoa za utotoni mkoani Shinyanga na kuwataka wananchi kuachana na imani za kishirikina huku akiwaomba viongozi wa dini na kimila kutoa elimu kwa wananchi kuachana na imani za kishirikina.
No comments