Breaking News

Rais MAGUGULI Akagua Unenzi Reli ya Kati Kwa Kiwango Cha Kisasa na Kuridhishwa na Maendeleo ya Ujenzi


Rais Dk. John Magufuli akifurahia jambo ndani ya Behewa la Treni ya Uhandisi alipokuwa akienda Mlandizi mkoani Pwani wakati akikagua kazi za ujenzi wa kipande cha Reli ya Kisasa kutoka Dar es salaam hadi Morogoro, leo. Ujenzi huo umefikia asililimia 80.

Na Mwandishi wa Ikulu
Rais Dk. John Magufuli leo 28 Juni 28, 2020 amekagua maendeleo ya ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge) kwa sehemu ya kwanza ya Dar es Salaam – Morogoro na kuelezea kuridhishwa kwake na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo mkubwa.

Rais Magufuli amesafiri kwa gari kandokando ya reli hiyo kuanzia Kisarawe hado Soga Mkoani Pwani na kisha akapanda kiberenge kilichopita katika reli hiyo mpya kuanzia Soga hadi Kikongo kabla ya kuendelea na safari yake kwa gari kuelekea Morogoro.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Masanja Kadogosa amemueleza Mhe. Rais Magufuli kuwa kazi ya ujenzi wa sehemu ya kwanza ya reli hiyo imefikia asilimia 82 ambapo Watanzania 13,000 wamenufaika na ajira na inatarajiwa kukamilika mwisho wa mwaka huu (2020).

Akizungumza na wananchi wa Soga na Kikongo, Rais Magufuli amewapongeza kwa kupata mradi huo na ametaka waendelee kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa ili waweze kunufaika zaidi na mradi huo.

Rais Magufuli amesikiliza kero za wananchi hao ambapo ameendesha harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya uboreshaji wa Shule ya Msingi Soga na kufanikiwa kukusanya sh. 68,535,000/- zikiwemo shilingi Milioni 5 alizochangia yeye mwenyewe, na amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kufika Kijijini hapo ili kutatua mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na mmiliki wa shamba kubwa lililopo kijijini hapo ambalo halilimwi na pia kumuagiza Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa kuhakikisha anatatua tatizo la maji linalokikabili kijiji cha Soga.

Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua madhubuti za kutekeleza mradi huo ambao utagharimu shilingi Trilioni 7.02 kwa sehemu ya kuanzia Dar es Salaam hadi Makutupora Mkoani Dodoma, pamoja na kutekeleza mradi mkubwa wa uzalishaji wa megawati 2,115 za umeme katika Bwawa la Nyerere ili kukuza uchumi wa Watanzania na kuinua kipato cha wananchi na hivyo amewataka Watanzania wote kuunga mkono juhudi hizo.

Akiwa Mlandizi, Rais Magufuli amesikiliza pia kero za wananchi na kumuagiza Naibu Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso kuhakikisha Wizara ya Maji inatatua tatizo la maji la Mitaa ya Mbwawa Shule na Mbwawa Mkoleni na pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe kuanza mchakato wa ujenzi wa barabara ya lami ya Mafia – Mzenga – Vikumbulu ili kuunganisha Mlandizi na reli.

Rais Magufuli amewasili Mjini Morogoro na kesho ataendelea na ziara yake Mkoani hapa ambapo ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa mahandaki ya reli ya kisasa (standard gauge) sehemu ya Morogoro – Makutupora, kuzindua barabara ya lami ya Rudewa – Kilosa na atafanya mkutano wa hadhara katika eneo Mkadage Wilayani Kilosa.

Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu (2020) huku wakikumbuka kudumisha amani, umoja na mshikamano pamoja na kuwachagua viongozi watakaowafaa

No comments