Breaking News

Mrema Ataja Mambo 5 Kati ya 21 Yanayoisukuma TLP Kumwunga Mkono Rais Magufuli Uchaguzi Mwezi Octoba.


Ndugu Watanzania wenzetu, Sisi wanachama, wafuasi na wapenzi wa chama cha Tanzania Labour Party ( TLP ) kwa kauli moja ya kizalendo kwa nchi yetu na kwa kuzingatia Ibara ya 29.0 ya Katiba ya Chama chetu Toleo la 2009 tumeamua kwa sauti moja kumuunga mkono mgombea wa chama cha Mapinduzi ( CCM ) Mhe Dk John Joseph Pombe Magufuli katika uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 25/10/2020 bila ahadi wala makubaliano yeyote baina yetu zaidi ya Uzalendo kwa Taifa letu la Tanzania,

Ndugu Watanzania wenzetu, Ifamike kuwa, azimio hili la kumuunga mkono Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli lilifikiwa baada ya kutafiti, kudadisi na kujiridhisha pasina shaka yeyote juu ya kazi zinazofanywa na Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli kuwa zinavunja rekodi zilizowekwa tangu enzi za mkoloni, zinaacha alama kwa kizazi hiki na kizazi kijacho, zinalipeleka Taifa kwa kasi kwenye Uchumi wa kati, zinadumisha Amani, Upendo na Mshikamamo wa Taifa letu na huu ndio ulikuwa mwanzao wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha tarehe 04/05/2019 pamoja na maazimio mengine kikao kiliazimia kila mjumbe/mwanachama apitie nukta kwa nukta kazi zinazofanywa na Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli kwenye ardhi ya Taifa hili la Tanzania.

Ndugu Watanzania wenzetu,Baada ya mwaka mmoja kupita, Kamati Kuu ya Chama na Halmashauri Kuu ya Chama ziliketi tena  tarehe 08/05/2020 Jijini Dar es salaam huku Agenda namba moja ikiwa ni “Tathimini ya Kazi zinazofanywa na Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli“ 98% ya wajumbe kwenye Kamati Kuu na 100% kwenye Halmashauri Kuu walitoa pendekezo la TLP kutoweka mgombea wa Urais bara na badala yake chama kimuunge Mkono Mgombea wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) Mh Dk John Pombe Joseph Magufuli.

Ndugu Watanzania wenzetu, Chombo cha juu kabisa cha maamuzi ya chama chetu cha TLP ni “Mkutano Mkuu wa TLP Taifa” ambao uliketi tarehe 09/05/2020 hapahapa Jijini Dar es salaam, Pamoja na wageni mbalimbali toka vyama rafiki alikuwepo pia Mhe Ndg Humphrey Polepole toka chama Tawala ambae ni “Katibu wa Itikadi na Uenezi” wa chama hicho aliyehudhuria kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM Mhe Dk Bashiru Ally Kakurwa na kwa umuhimu sana alihudhuria pia Naibu Msajili wa vyama vya Siasa nchini Mhe Systus Nyahoza.

Ndugu Watanzania wenzetu, Baada ya taarifa hiyo, Mnafahamu miongoni mwa malengo ya chama chochote cha Siasa ikiwemo Labour Party ni Kushika dola, Ishara ya chama kutaka kushika dola/serikali ni kuwa na Mgombea wa nafasi ya Urais wa JMT au SMZ, Sisi Labour Party chini ya M/kiti wetu mzalendo wa maneno na matendo Naibu Waziri Mkuu Mstaafu Mhe Dk Augustino Lyatonga Mrema tumekubaliana kwa sauti kuu “Tutamuunga mkono Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli kuelekea Uchaguzi mkuu wa Oct 2020 kwa hali na mali kama ishara ya Uzalendo wetu kwa Taifa letu kwa manufaa yetu sasa na manufaa ya watoto wa watoto wetu“

Ndugu Watanzania wenzetu, Ifahamike kuwa mpaka tarehe 09/05/2020 (siku ya mkutano mkuu) tayari tulishapokea nia za wanachama wawili ( 2 ) waliotaka kumkabili vikali Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli kwenye Uchaguzi mkuu wa Oct 2020 lakini Chama kupitia vikao vyake kimewashauri na wao kwa Uzalendo wao kwa nchi yao wamekubali kwa moyo safi kumuunga mkono na kumwachia Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli aendelee kwani yuko katika uelekeo wa “Kweli na Sahihi” kwa Taifa letu hili lililodumu na umasikini kwa muda mrefu tena bila sababu,

Ndugu Watanzania wenzetu, kwakuzingatia Imani ya nne ( 4 ) ya Labour Party inayosema “Kazi ni Msingi wa Demokrasia“ na kwa kuzingatia kazi kubwa na nzuri anazofanya Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli Sisi Labour party tunazitambua na kuzithamini kazi hizi kwa vitendo kwa kutoa chama chetu pendwa cha TLP  ( bara ) kama ishara ya Uzalendo wetu kwa nchi yetu ili kitumike kama nyezo ya kusaidia na kurahisisha ushindi wa Kishindo wa Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli kwenye nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pekee aidha chama chetu kitasimamisha wagombea wenye sifa madhubuti kwenye majimbo yote 264 na kata zote 3,956 wakati Zanzibar Mhe Hussuin Juma tayari ameshatangaza kugombea Urais wa SMZ kupitia chama chetu hiki pendwa cha Labour Tanzania.

Ndugu Watanzania wenzetu,Chama Chenu Cha TLP kwa unyenyekevu mkubwa kinawakaribisha wale wote wenyenia ya kumsaidia Mh Rais kwa kumnadi kwa Wananchi kupitia jukwaa la “Ugombea” kwenye nafasi ya Ubunge wa JMT na Udiwani ili mwisho wa siku ninyi na yeye kila mmoja atimize ndoto yake na wote kwa Umoja na Uzalendo wenu mkalijenge Taifa letu kwa kumsaidia Rais ajae Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli kupitia Bunge la 12 kama Wabunge wa JMT na Halmashauri zenu kama madiwani, Sisi TLP tunaamini kama Mgombea wetu wa Urais Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli atanadiwa na Wagombea wawili ( 2 ) katika kila Jimbo/Kata za JMT yaani yule toka chama chake cha CCM na wapili toka chama chetu cha TLP hakika ushindi atakaoupata utatikisa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania na hii ni kuionesha Dunia Uzalendo wetu katika kumpigania Mzalendo wetu wa kweli Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli Kabla,Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25/10/2020,

MAMBO 5 KATI YA 21 YANAYOISUKUSUMA ZAIDI LABOUR PARTY KUMUUNGA MKONO MHE DK JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI KUELEKEA 25 OCT 2020,

Watumishi 32,555 wenye dosari serikalini, Nyote Mtakumbuka March 2016 Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli  aliwaondoa watumishi wenye dosari wapatao 32,555 sawa 5% ya watumishi wote serikalini na hivyo kuokoa pesa za serikali kiasi cha Tshs 19.8bln katika kila mwezi hii ni sawa na Tshs 237.6bln kwa mwaka,Mpaka mwezi huu ( kwa miezi 51 ) Taifa kupitia yeye litakuwa limeokoa jumla ya Tshs 1.01trl zilizotafunwa bila huruma ambazo ni sawa na bajeti ya dawa kwa miaka 33 mfululizo kwenye Serikali ya awamu ya nne iliyofikia Tshs 31bln mwaka 2014/15,kiasi hiki cha fedha kilichookolewa ni sawa na kile  kilichotoa elimu bila malipo kwa miaka yote mitano ( 5 ) yaani Tshs 1.01trioni.

Ndugu Watanzania wenzetu,Hizi Tshs 1.01trl kupitia yeye zimetusaidia kuajiri vijana wetu 74,173 na kuongeza mishahara kwa njia ya kupandisha madaraja (Promotion) watumishi wapatao 306,917 sawa na 44% ya watumishi wote na ile hoja kwamba Mhe Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli hajaongeza mishahara kwa miaka 5 mfululizo kwa muktadha huu “Si ya kweli” kwani mfumo huu wa kuongeza mishahara kwa njia ya kupandisha madaraja ni bora zaidi ya ule wa ongezeko la lazima la mshahara ( statutory annual salary increment ) ambapo kimataifa ( ILO ) ni kati ya 1-3.1% tu kwa mwaka ukilinganisha na huu wa kukua kwa TGS.

Ndugu Watanzania wenzetu, Hizi Tshs 1.01trl kupitia yeye zimetusaidia kulipa madeni ya watumishi yaliyohakikiwa yasiyo ya kimishahara na yakimishahara yenye thamani ya Tshs 472.6bln, Sisi Labour Party,katika vikao vyetu hivyo tulitafakari sana juu ya jambo hili,Kama mtu anaweza kuokoa pesa ya serikali inayofikia Tshs 1.01 trl iliyokuwa inatafunwa bila huruma hivi Sisi ni nani hata tusimuunge mkono mtu wa aina hii! Na ninyi wengine mnasubiri nini kumuunga mkono Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli kuelekea oct 2020 ili kushuhudia maajabu zaidi !?

Usambazaji wa Umeme vijijini ( REA ) Ndugu Watanzania wenzetu,Wakati Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli anaingia madarakani mwaka 2015 palikuwa na vijijini 2,018 tu vyenye umeme nchi nzima,kwa lugha rahisi tangu Tanzania iumbwe ni vijiji 2,018 tu kati ya vijiji 12,268 sawa 17% ndio vilikuwa na umeme kabla ya ujio wa Mhe Dk John Pombe Magufuli kama Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania Nov 2015.

Ndugu Watanzania wenzetu,Mpaka  tarehe 09/05/2020 tunatangaza kumuunga mkono Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli bei ya kuunganisha umeme ilifikia Tshs 27,000/= tu toka Tshs 177,000/= mwaka 2015, Kwa bei na miaka hii minne na nusu jumla ya vijiji 9,112 sawa na 74.3% sawa na ongezeko la vijiji 7,094 vilikuwa vinawaka umeme, Mpaka tunatoa tamko hili ni vijiji 3,156 tu sawa na 25.73% ndio bado havijafikiwa na umeme ili kufanya Tanzania yote kumeremeta kwa Umeme wa uhakika.

Ndugu Watanzania wenzetu, Mfahamu pia uzalishaji wa Umeme umeongezeka toka 1,038MW mwaka 2015 hadi 1,602 MW mwaka huu sawa na ongezeko la 564 MW sawa na 54.34% wakati huohuo Umeme toka maporomoko ya Rufiji ( SG ) wenye kuzalisha karibu 2,115 MW ukisubiriwa ili kuifanya Tanzania kuwa na vyanzo vya umeme vinavyofikia 3,717 MW Umeme utakaotulazimu pia kuwauzia majirani zetu, Mpaka sasa watumiaji wa umeme nchini wamefikia 85% toka 35% mwaka 2015 sawa na ongezeko la 50%, kwa haya yote, hivi Sisi Labour party ni nani hata tusimuunge mkono mtu wa aina hii na ninyi wengine mnasubiri nini kumuunga mkono Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli kuelekea oct 2020?

Ujenzi wa miundombinu ( infrastructure)

Ndugu Watanzania wenzetu,Kabla ya kumuunga mkono Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli tulipitia ripoti ya “The Africa Construction trend report 2019” ya Deloitte Consultancy Firm, Tanzania na Kenya walisajiri miradi mikubwa  51 kila moja isipokuwa thamani ya miradi ilitofautiana baina yao, Miradi 51 toka nchi ya Kenya ilikuwa na thamani ya $ 36 bln sawa na 24.6% ya thamani ya miradi yote 182 ambayo ni $146 bln na miradi 51 ya Tanzania ilikuwa na thamani ya $60.3 bln sawa na 41.2% au Tshs 140 trl ya thamani ya miradi yote.

Ndugu Watanzania wenzetu, Sisi TLP tulishangaa sana Kwa miaka zaidi 35 ni Kenya na Ethiopia pekee ndio zimekuwa nchi zinazoongoza kwa kurekodi miradi mingi na mikubwa yenye thamani kubwa katika Ukanda wa nchi za Africa ya Mashariki, Tanzania pamoja na rasilimali zetu lukuki hatukuwahi kufikiriwa  kuwa ipo siku tutaongozi kwa miradi ya thamani kubwa Ukanda mzima wa Africa Mashariki wenye nchi za Kenya, Ethiopia, Uganda, Rwanda, Burudi, Shelisheli, Djibout, Somalia, Comoro na Elitrea.

Ndugu Watanzania wenzetu,Nibaada ya karibu nusu karne ni kwa mara ya kwanza Tanzania inarekodi miradi yenye thamani kubwa zaidi ya Eikthiopia & Kenya vinara wa miradi mikubwa na yenye thamani kubwa kwa miaka 35 na hili linafanyika chini ya Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli huku jumla ya thamani ya miradi yetu ikifikia 41.2% ya miradi yote ambayo ni karibu sawa na nusu ya thamani ya miradi yote 182 yenye jumla ya $146bln kwa lugha rahisi kazi inayofanywa na Rais mmoja wa Tanzania ni karibu sawa na nusu ya kazi yote inayofanywa na marais wote kumi ( 10 ) toka nchi za Kenya, Ethiopia, Elitrea, Uganda, Rwanda, Burundi, Comoro, Somalia, Shelisheli na Djibou 
ti,hapa yupo pia Uhuru Kenyatta wa Kenya.

Ukuaji wa Sekta ya Elimu nchini,
Ndugu Watanzania wenzetu,Mfahamu kuwa sisi pia tunawatoto wanaosoma katika shule zetu za Awali, Msingi na Sekondari, Baada ya Tangazo la Elimu bila Malipo mapema mwaka 2016 kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto kujiunga na shule zetu katika ngazi mbalimbali, Hadi tunatangaza kumuunga mkono Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli tarehe 09/05/2020 watoto wetu na watoto wa masikini wenzetu wastani wa wanafunzi1.6M wamejiunga mwaka huu tofauti na wale 1.0M waliojiunga mwaka 2015, Kwa lugha rahisi elimu bila malipo ya Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli imekuja na wastani wa watoto 600K zaidi kila mwaka au wastani wa watoto 3M kwa miaka hii mitano ya kwanza,Kwa matokeo haya, Sisi Chama cha Labour ni nani hata tusimuunge mkono Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli na mnaosema tumenunuliwa ninyi Uzalendo wenu uko wapi kwa Taifa lenu? 

Ndugu Watanzania wenzetu, Jumla ya shule mpya za msingi 905 zimejengwa kwa miaka hii minne na nusu na kufikia jumla ya shule 17,804 mwaka huu toka shule 16,899 mwaka 2015,Huku shule zingine mpya 622 za Sekondari pia zikijengwa na kufikia jumla ya shule 5,330 kutoka shule 4,708 mwaka 2015,Na Shule zote kongwe 89 zimekarabatiwa isipokuwa 16 tu sawa na 18%,Mabweni 253 na vyumba vya maabara 227 pia vilijengwa,kwa lugha rahisi jumla ya majengo mapya 2,007 yakujifunzia yamejengwa na Mhe Dk John Joseph Pombe Magufuli kwa muda huu mfupi wa awamu yake ya kwanza, Tutafakari kwa pamoja ni nini kitatufanya tusimuunge mkono mtu huyu kwa kazi hizi na iweje mtu anayeunga mkono haya tuseme kanunuliwa!? tuendelee kutafakari na kujitafakari kizalendo tena na tena.

Ndugu Watanzania wenzetu, Mikopo ya Elimu ya Juu imepandwa kwa Tshs 101.3bln yaani kutoka Tshs 348.7bln mwaka 2015 hadi Tshs 450bln mwaka 2020, Jumla ya wanafunzi wapya 32,583 wameongezwa na hivyo kufanya jumla ya wanafunzi wanaopata mkopo kufikia130,883 mwaka 2020 toka wanafunzi 98,300 mwaka 2015 huku wanafunzi wa Sekondari ( I-IV ) wastani wa wanafunzi 537,000 wakiongezeka na kufika wanafunzi 2.185M mwaka 2020 ukulinganisha na wanafunzi 1.648M haya yote yakiwa ni matokeo ya Tshs 1.01 trl fedha za elimu bila malipo toka kwa Mhe Dk John Joseph Pombe Magufuli haya ndio yanatufanya sisi chama makini cha Labour Tanzania,

Kuimarika kwa Huduma za Afya nchini.
Ndugu Watanzania wenzetu, Upatikanaji wa damu salama umeongezeka na kufikia lita 309,376 kwa mwaka 2020 toka lita 104,632 mwaka 2015 sawa na ongezeko la lita 204,744 ikiwa ni sawa na 196%, ndio sababu vifo vya watoto wachanga vimepungua na kufikia vifo 7 kutoka 25 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2015, Wakati huohuo WHO wanasema  mwaka 2019 maambuzi ya Malaria yalipungua kutoka 14% mpaka 7%  ( Single digit ) maana yake Tanzania sasa Chini ya Mhe Dk John Joseph Pombe Magufuli malaria imeshuka kwa 50%, Huku Bajeti ya dawa nayo ikifikia Tshs 270bln toka Tshs 31bln mwaka 2015 ikiwa ni sawa na ongezeko la Tshs 239bln mwaka 2020 sawa na 771%, Watanzania wenzetu, Hivi kwa haya yanayofanyika sasa TLP ni nani hata tusiyaone haya, na iweje tukiunga mkono iwe ni nongwa kwenu,? Ninyi Uzalendo maana yake nini kama si huu wa kusimama nanchi yetu!?

Ndugu Watanzania wenzetu,Mmeona na kushudia Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli akijenga hospitali tatu ( 3 ) za rufaa, za mikoa kumi ( 10 ), za wilaya sabini na moja ( 71 ),vituo vya Afya 487,Zahanati 1,198 na kufanya Jumla ya Vituo vipya vya kutolea huduma vilivyojengwa awamu ya kwanza pekee kufikia 1,769 na kufanya jumla ya vituo vya kutolea huduma za Afya Tanzania kufikia 8,783 mwaka 2020 toka vituo 7,014 mwaka 2015,Ukitafuta uwiano wa vituo hivi  dhidi ya Idadi ya watanzania ambao tunakadiriwa kufikia 55M, yaani 0.009M : 55M sawa na 1:6,111 yenye maana kila Kituo kimoja cha kutolea huduma ya Afya Tanzania kitahudumia wangonjwa 6,111 kwa mwaka, Hii ni sawa na  wagonjwa 6,111/366 kwa siku, Hii ni sawa na kusema 1:17, Kila Kituo kimoja cha kutolea Afya kitahudumia Wagonjwa Kumi na saba ( 17 ) tu kwa siku na hili limewezekana chini ya Uongozi madhubuti wa Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli, Sisi Labour Party baada ya kuona haya yote yakitokea Chini yake Rais wetu makini na Mpenda watu hasa Wanyonge na wanaodharaulika tumekubaliana kuungana na chama chochote cha Siasa kwa Sharti kwanza lakumuunga mkono Mhe Dk John Joseph Pombe Magufuli kwa kutangaza hadharani kama tunavyofanya sisi, Pili sisi TLP tutazunguka nchi nzima kumnadi Mgombea wetu Mhe Dk John Pombe Joseph Magufuli na kwa Unyenyekevu mkubwa tuwaombe kila anayedhani kuwa ni Mzalendo wa kweli wa Taifa letu asimame na Rais Magufuli kufa au kupona kwa jasho au kwa damu kuhakikisha mzalendo wetu anasalia madarakani.

Pamoja na salama za Chama chetu,Tunamtakia afya njema Mgombea wetu na kipekee kabisa tunamkaribisha Makao Makuu ya Chama Chetu ili kututembelea.

MHE DK AUGUSTINO LYATONGA MREMA,
MKT WA TLP TAIFA,
24/6/2020.

1 comment: