Tanzania Yasaini Mkataba Wa Kupatiwa Fedha Za Msaada Bilioni 60 Za Kitanzania Kutoka Serikali Ya China
Tanzania imetia
saini Mkataba wa kupatiwa fedha za Msaada wa Shilingi Bilioni 60 za kitanzania
kutoka Serikali ya Watu wa China bila ya masharti yeyote ambapo Serikali ya
Tanzania itaamua matumizi yake katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwa
wananchi wake.
Mkataba huo
umesainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof.
Palamagamba John Kabudi ambaye ameiwakilisha Serikali ya Tanzania na
Makamu Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la China Bw.
Zhou Liujun kwa upande wa Serikali ya China. Mkataba huo umesainiwa punde tu
mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo kati ya Waziri Prof Palmagamba
John Kabudi na Waziri wa Mambo ya Nje wa China na Mjumbe wa Baraza la Taifa
Mhe. Wang Yi.
Mazungumzo ya
Mawaziri hao yalilenga kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia baina ya China na
Tanzania sambamba na kuibua maeneo ya kipaumbele na kimkakati
yatakayotekelezwa kwa ushirikiano baina ya China na Tanzania.
Maeneo hayo ni
pamoja na upembuzi yakinifu kwa ajili ya upanuzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete ili kuwa Taasisi Mahiri ya Tiba ya Moyo Kusini mwa Jangwa la
Sahara, ujenzi wa mabwawa ya kuzalisha umeme ya Ruhudji (megawatt 358) na
Rumakali (megawatt 222) mkoani yaliyoko mkoani Iringa na Njombe ambayo yote kwa
pamoja yatakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa takribani megawati 580,pamoja na
upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (standard
gauge railway) sambamba na ukarabati wa reli ya TAZARA.
Aidha, katika
mazungumzo yao, Serikali ya China imeahidi pia kuunga mkono katika ujenzi wa
miundombinu muhimu katika mji mpya wa Serikali katika makao makuu Dodoma.
Waziri wa Mambo ya
Nje wa China na mjumbe wa Baraza la Taifa Mhe. Wang Yi amesifu mahusiano mema
na ya kirafiki baina ya Tanzania na China na kuongeza kuwa Tanzania imekuwa
Rafiki wa kweli wa China kwa wakati wote.
Kwa upande wake
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba
John Kabudi ameishukuru Serikali ya China sambamba na kueleza kuwa kipaumbele
cha Tanzania ni kudumisha na kuendeleza mahusiano mazuri ya
kidiplomasia,kisaiasa na kiuchumi yaliyopo baina ya Nchi hizo mbili kwa manufaa
ya pande zote mbili.
Pia Prof. Kabudi
ameipongeza Serikali ya China na Nchi za Afrika kwa kuandaa mpango kazi wa kimkakati
ambao umeanisha maeneo kumi ya kipaumbele yakiwemo uendelezaji wa sekta ya
viwanda na miundombinu ambayo kwa nchi za Afrika hususan Tanzania ndio
kipaumbele cha kwanza. Maeneo mengine ya kipaumbele ni pamoja na uendelezaji wa
biashara na uwekezaji kati ya China na Afrika pamoja na ushirikiano katika
maeneo ya ulinzi na usalama kwa kutaja machache.
Halikadhalika, Prof
Kabudi ameisifu Serikali ya China kwa kubainisha hatua kubwa nane
zitakazosaidia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Beijing (2019 – 2021). Miongoni
mwa hatua hizo ni pamoja na kuanzisha program maalum ya ujenzi wa maeneo maalum
ya viwanda (Industrial park), ujenzi wa miundombinu ya nishati, usafirishaji na
mawasiliano,mpango maalum wa ujenzi wa vyuo vya ufundi na vituo vya kutolea
mafunzo ya stadi kwa ajili ya kuandaa nguvu kazi ya kufanya kazi viwandani.
Katika hatua
nyingine Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof.
Palamagamba John Kabudi amehudhuria mkutano kati ya mawaziri wa mambo ya nje
kutoka nchi 53 za Afrika na taasisi za fedha za China ambazo ni pamoja na Mfuko
wa Maendeleo kati ya China na Afrika (CAD FUND), Benki ya Exim ya China pamoja
Benki ya Maendeleo ya China yenye lengo la kutoa ufafanuzi na utaratibu wa
fedha kiasi cha Dola bilioni 60 zilizoahidiwa na Serikali ya China wakati wa
Mkutano Mkuu wa Wakuu wa Nchi za Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika
(FOCAC) uliofanyika mwezi Septemba, 2018 jijini Beijing.
Awali, katika ya
ufunguzi wa mkutano huo,mchumi mkuu wa Benki ya Maendeleo ya China Liu Yong
amesema China ina matumaini makubwa kuwa Afrika itaendelea kiuchumi na kwamba
wataendelea kushirikiana na Nchi zote kwa kuwa malengo yao ni kuona nchi za
Afrika zinaendelea kupitia ushirikiano baina ya China na Afrika.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
BEIJNG - CHINA.
24 Juni 2019
No comments