Breaking News

TIC chamshukuru JPM kwa kukipigania kihamasishe uwekezaji, kukipatia jengo la ofisi chatoa wito kwa taasisi na mamlaka kuacha kufunga biashara za wawekezaji


Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) kimemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa jitihada za kukipigania ili kiendelee kuhamasisha na kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali pamoja na kukipatia Jengo jipya la Ofisi lililotakiwa litumiwe na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Aidha, kituo hicho kimetoa wito kwa taasisi na mamlaka husika kuacha kufunga biashara za wawekezaji badala yake zitumie njia za busara katika kutatua changamoto za wawekezaji zinazojitokeza.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaan na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Geoffrey Mwambe wakati akitoa ufafanuzi kwa wanahabari.

Amesema katika ziara alizozifanya Rais Magufuli mkoani hivi karibuni hasahasa katika mikoa ya Ruvuma na Njombe Rais Magufulli ameonyesha nia ya dhati ya kukipigania kituo hicho ili kipige hatua na kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kuratibu na kuhamasisha uwekezaji nchini na kwamba kimpokea kauli ya rais ya kukitaka kuzifanyia baadhi ya sheria. marekebisho.

" Kituo kinapenda kuchukua fursa hii kumshukuru Rais Magufuli kwa kutupigania akiwa katika mikoa ya Ruvuma na Njombe ameonyesha jinsi gani anataka tupige hatua katika kutekeleza majukumu yetu," amesema Mwambe.

Amebainisha kuwa Rais Magufuli akiwa katika ziara yake alihamasisha nchi kutumia rasilimali zake na kuondokana na fikra za kutegemea misaada na kwamba kupitia uhamasishaji uwekezaji inawezekana kuondokana na dhana hiyo.

Amesisitiza kuwa kituo hicho kinamuahidi Rais Magufuli kuendelea kutekeleza majukumu kikamilifu pamoja na kushirikiana Waziri Mkuu na taasisi nyingine lengo likiwa kuondoa ukwamishaji wa wawekezaji nchini.

Amefafanua kuwa ili nchi ifanikiwe kutekeleza miradi mikubwa ikiwemo ya ujenzi wa vyuo vikuu, tafiti na Mradi wa Stiglers Gorge  lazima kodi ikusanywe kupitia uwekezaji na kuongeza idadi ya walipakodi.

Mwambe ametoa wito kwa taasisi na mamlaka husika kuacha kufunga biashara za wawekezaji zikiwemo hoteli, ofisi na viwanda na kwamba zitumia busara kuwapa maagizo na sio kuwakomoa hali inayoweza kuikosesha nchi kodi.

"Taasisi zijizuie kufunga biashara za wawekezaji kuna njia za kufuata ikiwemo mazungumzo na maagizo kuwafungia kunasababisha hasara kubwa kwani kampuni zinazolipa kodi kwa siku kwa Serikali," amesema Mwambe.

Katika hatua nyingine amesema kuwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Uwekezaji  litakalofanyika kuanzia Mei 2 hadi 9 mkoani Kigoma huku akibainisha kusajili miradi 80 ya uwekezaji kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka huu.

Amesema kongamano hilo litashirikisha waoneshaji zaidi ya 150 kutoka nchi za Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Burundi, Rwanda na Zambia na kwamba litalenga sekta ya viwanda, kilimo na kuziongezea thamani biashara.

Wakati huo huo, amesema katika miradi 80 iliyosajiliwa kati yao 49 ni ya viwanda, 11 ya usafirishaji na sita ya sekta ya utalii.

TIC chamshukuru JPM kwa kukipigania kihamasishe uwekezaji, kukipatia jengo la ofisi chatoa wito kwa taasisi na mamlaka kuacha kufunga biashara za wawekezaji

No comments