Breaking News

Asasi Za Kiraia Na Wanachama Wa Mtandao Wa Watetezi Wa Haki Za Binadamu Nchini Walaani Mauaji Ya Watoto 10 Mkoani Njombe.

Asasi za Kiraia na wanachama wa Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu nchini (THRDC) wamelaani mauaji ya watoto kumi yaliyotokea huko mkoani Njombe ambapo kwa mujibu wa Taarifa ya Jeshi la Polisi chanzo kikuu ni imani za kishirikina.

Akisoma tamko kwa niaba ya Asasi hizo Jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Kituo cha sheria na Haki za binadamu Bi. Anna Henga alisema kumekuwa na ongezeko la Vitendo vya ukatili dhidi ya Watoto ambavyo hupelekea kukosesha mtoto ustawi na ukuaji bora ambapo mwaka 2018 jumla ya matukio 6376 yaliripotiwa.

"Katika kipindi cha hivi karibuni yamekuwa yakiripotiwa matukio ukatili dhidi ya Watoto kutekwa kisha kuwafanyia unyama na kusababisha vifo vyao huku wakiwachukuwa baadhi ya sehemu za viuongo vya miili yao licha ya jitihada zinazofanywa na Jeshi la Polisi nchini pamoja na wananchi"Alisema Bi Henga.

Kwa upande wake Bi. Monica Alex akielezea tukio hilo alisema Mauaji yaliyotokea Mkoani Njombe yanapaswa kukemewa vikali na kila mmoja, Serikali, Asasi watetezi wa haki za binadamu na wadau wengine na kusisitiza jamii kuheshimu haki za Watoto kwani ni jukumu la kila mmoja kuwalindwa dhidi ya vitendo vya kikatili.

"Nitoe wito kwa jamii kuwa mstari wa mbele kulinda na kutetea haki za mtoto na yeyote atakayebainika anazivunja katika mazingira hatarishi ama haki zake zinavunjwa au inaekekea kuvunja atawajibishwa kisheria" Alisema Bi Alex

Mtandao wa Asasi za kiraia na wanachama wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu nchini inaundwa na taasisi 20 zisizo za kiserikali.

No comments