Waziri Mwakyembe: Kanuni Mpya Kudhibiti Matusi Na Picha Za Uchi Mitandaoni
Serikali imesema kanuni mpya za
maudhui kwenye mitandao, runinga na redio zimetungwa kwa lengo la kudhibiti
usambazaji wa kauli chafu, matusi, picha za utupu na zenye maudhui yasiyofaa
kwa watoto.
Kanuni hizo zimetungwa ikiwa ni
utekelezaji wa Sheria ya Mawasiliano ya Kiektroniki na Posta ya Mwaka 2010.
Pia imesema itaendelea kuhamasisha
utengenezaji na uzalishaji wa maudhui ya ndani yanayozingatia maadili, mila na
desturi za Mtanzania huku ikikiri kuwapo kwa mmomonyoko wa maadili
kunakoongezeka siku hadi siku, hivyo imejipanga kukabiliana na changamoto hiyo.
Akiwasilisha bungeni mjini hapa jana
hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Waziri wa wizara hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe, alisema kanuni hizo zinamtaka
kila mtumiaji wa mitandao awe na namba ya siri ili 'wajanja' wasitumie kirahisi
chombo chake cha mawasiliano kutenda matendo yanayokwenda kinyume cha sheria.
Alisema kanuni hizo pia zinaweka muda
maalumu kwa picha mgando na nyongevu za filamu au muziki wenye maneno yasiyofaa
kwa watoto kuonyeshwa kwenye runinga.
"Tuliweka muda huo maalumu
kuanzia saa 4:00 usiku hadi saa 11:30 asubuhi, lakini wadau wamekuwa wakali,
wanadai picha na nyimbo hizo zirushwe kuanzia saa 6:00 usiku wakati watoto
wamelala na mwisho saa 11:00 asubuhi, kabla watoto hawajaamka," alisema
Dk. Mwakyembe.
Aliongeza kuwa kanuni hizo zinataka
madaraja yawekwe kwa kila filamu, video, wimbo au albamu kutoka ndani au nje ya
nchi ndipo kazi hizo zitumike kwenye vyombo vya utangazaji.
"Msingi wa kanuni hizi ni
kuhakikisha teknolojia inatutumikia badala ya kututumikisha na kuvuruga
mustakabali wa maadili ya taifa letu. Ni kanuni zilizozingatia mazingira yetu
halisi kama kila Watanzania," alisema.
Dk. Mwakyembe alisema, mmomonyoko wa
maadili ya Kitanzania unaoongezeka siku hadi siku, ni miongoni mwa changamoto
zinazoikabili wizara yake.
Alisema wanaendelea kutoa elimu
kupitia vyombo vya habari na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia
maadili, mila na desturi za Kitanzania.
Ili kutekeleza majukumu yake kwa
mwaka ujao wa fedha, Dk. Mwakyembe aliliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Sh.
bilioni 33.3. Kati yake, Sh. bilioni 12.2 ni mishahara, Sh. bilioni 9.3 kwa
ajili ya matumizi mengine na Sh. bilioni 8.7 za utekelezaji wa miradi ya
maendeleo.
No comments