Magereza Wataja Sababu Za Kumzui Profesa Jay Kumuona Sugu Gerezani
Mbunge wa Mikumi mkoani Morogoro,
Joseph Haule ‘Profesa Jay’ jana alizuiwa kumuona mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph
Mbilinyi pamoja na katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel
Masonga baada ya kuzuiwa na maofisa wa magereza.
Profesa Jay aliyeambatana na mke
wake, Grace Haule walifika jana jijini Mbeya na kwenda gerezani kuwaona Sugu na
Masonga ambao wapo mahabusu wakikabiliwa na kesi ya kutumia lugha ya fedheha
dhidi ya Rais John Magufuli.
Mkuu wa magereza Mkoa wa Mbeya,
Kamshina Msaidizi Mwandamizi (SACP), Paul Kijida alisema walimzuia Profesa Jay
kwa sababu haikuwa siku ya kuwaona mahabusu.
‘Kweli amekuja hadi ofisini kwangu,
lakini taratibu hazipo hivyo. Siku za kawaida kama hizi tunamruhusu mtu
anayempelekea chakula au ataruhusiwa pale mfungwa au mahabusu anaumwa au
mwanasheria wake anaruhusiwa kama tu kuna kitu muhimu’’ alisema Kijida na
kuongeza kwamba,
‘’Lakini tukisema kila mtu kwa muda
na siku anayotaka iwe siku ya kuwaona wafungwa au mahabusu hatutafanya kazi
sasa. Siku za kuwaona wafungwa na mahabusu kwa watu wa kawaida ni Jumamosi na
Jumapili tu,” alisema mkuu huyo wa magereza.
‘’Nimejaribu kuonana na RPO (mkuu wa
magereza mkoa) lakini naye ameonekana kusita kunipa kibali cha mimi kuonana
nao.
"Na inaonyesha kuna kitu nyuma
kimejificha. Lakini nimefunga safari kuja kuonana nao hivyo siwezi kuondoka
bila kuonana hivyo kesho(leo) nitakuwepo mahakamani, nitazungumza nao,” alisema
Profesa Jay jana.
Alisema anachotambua ni kuwa mbunge
hazuiliwi kuwaona mahabusu gerezani, lakini jambo hilo limemshangaza.
Akizungumza na mama yake Sugu aitwaye
Desderia, alimtaka kuwa na ustahimilivu katika kipindi hiki ambacho mwanaye
yupo kwenye misukosuko.
Profesa Jay alisema, “mama usihofu,
yule hajabaka wala hajaiba bali kilichomuweka ndani ni kutetea masilahi ya
wananchi. Na ndio maana hata sisi tumeacha kazi zote huko kuja kuhakikisha
tunashughulikia jambo hilo na naamini haki itatendeka tu.
"Na hapa usione tupo wachache
kuja hapa nyumbani, lakini Sugu ana kundi kubwa sana la watu na tumegawana
majukumu ya kufanya kuhusu hili tatizo.”
No comments