Rugemalira wa Escrow agonga mwamba Mahakama ya Mafisadi
MSHITAKIWA wa kesi ya uchotaji
fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow, James Rugemalira amegonga ukuta katika
Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi (Mahakama ya
Mafisadi) baada ya kunyimwa dhamana.
Rugemalira ambaye anakabiliwa na
kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, yenye mashtaka ya
utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana, alikimbilia mahakamani hapo kuomba
afutiwe mashtaka ya utakatishaji fedha kisha
aachiwe huru kwa dhamana kwa madai hati ya mashtaka yanayowakabili ina kasoro
za kisheria.
Jana,
Jaji Mfawidhi Firmin Matogolo alitupilia mbali maombi hayo akisema Mahakama
hiyo haina mamlaka ya kumpa nafuu alizokuwa akiziomba.
Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, jopo la mawakili wa
Rugemalira waliieleza Mahakama kuwa hati ya mashtaka haina maelezo yanayoonyesha
kosa la utakatishaji fedha.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Dk Zainabu Mango alipinga
hoja hizo, akidai mashtaka yanayomkabili mshtakiwa hayana dhamana.
Akijibu hoja ya kasoro za hati ya mashtaka, Wakili Mango alidai
maombi hayo yamepelekwa kwenye jukwaa ambalo si sahihi.
Alisema kesi hiyo haijafikia hatua ya kusikilizwa katika
mahakamani hiyo na kwamba inaweza kuangalia uhalali wa mashtaka hayo, shauri
hilo litakapohamishiwa mahakamani hapo kwa usikilizwaji.
Hata hivyo, Jaji alikubaliana na hoja za Wakili Mango kuwa
Mahakama hiyo haina mamlaka ya kuchunguza uhalali wa hati ya mashtaka kwa kuwa
suala hilo limefikishwa wakati ambao si muafaka.
Pia, Jaji Matogolo alisema kwamba Mahakama hiyo huwa na mamlaka
ya kuchunguza uhalali wa mashtaka endapo maombi yangewasilishwa kwa njia ya
mapitio na si dhamana.
Rugemalira na mshirika wake wa Kampuni ya kufua umeme ya
Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Harbinder Singh Sethi wanakabiliwa
na kesi ya uhujumu uchumi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
No comments