Waziri Mkuu Agomea Ombi La Wabunge Wa Tabora
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amekataa ombi la wabunge wa Ulyankulu na Kaliua ya mkoani Tabora ya kuigawa
Wilaya ya Kaliua ili kusogeza huduma kwa wananchi waishio kwenye kata na tarafa
zilizo mbali.
Hii si mara ya kwanza kwa
kiongozi wa juu wa Serikali kutamka hadharani kwamba hawatagawa maeneo mapya
utawala.
Julai mwaka jana akiwa katika
ziara ya kikazi katika mkoa huo, Rais John Magufuli pia alikataa ombi la
kuugawa Mkoa wa Tabora akisema haoni umuhimu wa kufanya hivyo na badala yake
fedha hizo zielekezwe katika kuboresha miundombinu ya barabara, maji na huduma
za afya.
“Nataka huduma kwanza mkoa
baadaye, huwezi ukaigeuza kila wilaya ikiwa mkoa. Kila unapotengeza mkoa
Serikali inaingia gharama. Ninataka niseme ukweli ni nafuu tutekeleze ahadi
kwanza,” alisema Rais Magufuli katika ziara hiyo.
Awali, Februari mwaka huu, Rais
Magufuli aliridhia kuanzishwa kwa wilaya mpya za Songwe, (Mkoa wa Songwe),
Kibiti (Pwani), Kigamboni na Ubungo (Dar es Salaam), Malinyi (Morogoro) na
Tanganyika (Katavi).
Kabla ya kutangaza wilaya hizo,
mwaka 2015, Serikali iligawanya baadhi ya majimbo mbalimbali kutokana na ukubwa
na kupata majimbo mapya 26.
Miongoni mwa majimbo hayo ni
Kibamba, Kigamboni, Makambako, Butiama, Tarime Mjini, Bunda Mjini, Tunduma,
Newala Mjini, Mbagala, Vwawa, Mafinga Mjini, Nanyamba, Handeni Mjini, Ushetu,
Nzega Mjini, Ndanda na Madaba.
Jana, akiwa katika mikutano ya
hadhara iliyofanyika Ulyankulu na Kaliua ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya
kikazi katika Mkoa wa Tabora, Majaliwa aliwaambia wananchi na wabunge hao
kwamba Serikali imesitisha mchakato kutoa maeneo mapya ya utawala hadi
itakapotangazwa vinginevyo.
Akijibu maombi ya wabunge hao
Magdalena Sakaya (Kaliua) na John Kadutu (Ulyankulu), ambao walisema kuna haja
ya kuigawa Wilaya ya Kaliua ili kusogeza huduma kwa wananchi waishio kwenye
kata zilizo mbali na tarafa Majaliwa alisema, “Tumesitisha kutoa maeneo mapya
ya utawala ili tuimarishe kwanza yale ya awali. Tunaimarisha kwanza miundombinu
ya majengo ya ofisi, nyumba za watumishi kwenye wilaya na halmashauri mpya,
zikitengamaa tutafanya uamuzi upya.”
Kuhusu migogoro baina ya
wanavijiji na maeneo ya hifadhi, Majaliwa alisema Serikali bado inafanya
uhakiki wa mipaka katika maeneo ya hifadhi na ikikamilisha mchakato huo na
itatoa taarifa.
Ili kuharakisha mchaktato huo,
Majaliwa aliwataka wananchi wanaoishi pembezoni mwa vijiji vinavyopakana na
maeneo ya hifadhi wasifanye upanuzi wowote hadi uhakiki wa mipaka
utakapokamilika.
“Tumeamua kuweka beacons katika
maeneo yote ya hifadhi ili kubaini mipaka imepita wapi. Wananchi mkiwaona watu
wa hifadhi wanapita huko msigombane nao. Ni hatua ya awali ya kubaini maeneo ya
mipaka,” alisema.
Awali Mbunge wa Kaliua (CUF),
Magdalena Sakaya alimweleza Majaliwa kwamba wananchi wanashindwa kujenga makazi
ya kudumu katika maeneo waliyopo kwa sababu wanatishiwa kwamba wapo hifadhini.
Hata hivyo, Majaliwa alisema
Serikali inafanya mapitio na ikilazimu, itabidi ifanye marekebisho ya sheria
inayohusu Misitu ya Hifadhi pamoja na sheria inayohusu masula ya wakimbizi.
No comments