Rais Magufuli Aridhia Kupokonywa Shamba La Sumaye
Waziri Mkuu wa mstaafu,
Frederick Sumaye ameingia matatani tena baada ya Halmashauri ya Wilaya ya
Mvomero kumpokonya shamba lake lenye ukubwa wa ekari 326 kwa madai ya
kutoendelezwa huku ikisema Rais John Magufuli ameridhia hatua hiyo.
Hili ni shamba la pili Sumaye
kunyang’anywa baada ya ekari 33 zilizopo eneo la Mabwepande kuchukuliwa Novemba
mwaka jana huku Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi akisema Serikali
ilifikia uamuzi huo baada ya kiongozi huyo mstaafu kushindwa kuliendeleza kama
notisi ya siku 90 ilivyoeleza.
“Oktoba 28, mwaka huu, Rais
John Magufuli alibatilisha hati ya kumiliki ardhi ya shamba namba 3,074
lililopo Mabwepande. Shamba hilo lilikuwa na hati namba 53086. Jina la mmiliki
lililoandikwa katika hati ni Frankline Sumaye,” alisema Hapi.
Jana, Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Mvomero, Frolent Kyombo alisema Rais Magufuli amekubali kufutwa kwa umiliki
wa shamba hilo kupitia ilani ya ubatilisho ya Mei mwaka huu.
Kabla ya kupokonywa shamba
hilo, Kyombo alisema Sumaye alipewa notisi ya siku 30 iliyomtaka kueleza sababu
za kutoendeleza matumizi ya shamba hilo kwa shughuli za kilimo kama
lilivyosajiliwa lakini hakutoa sababu zilizoweza kushawishi kutofanyika kwa mabadiliko
hayo.
“Hatua ya pili, tukatoa ilani
ya ubatilisho wa shamba hilo, kuna maelezo alitoa lakini tuliona hayakuwa na
uzito, tukayatupilia mbali, shamba hilo alikuwa anaendesha shughuli za kilimo
pamoja na ufugaji. Alikuwa anatumia asilimia 15 hadi 20 tu ya shamba lote,”
alisema Kyombo.
Alisema mbali na kutumia sehemu
ndogo huku nyingine ikiwa haitumiki, Mwenyekiti huyo wa Chadema Kanda ya Pwani
alikuwa amekiuka Sheria ya Mipango Miji, namba 8 ya mwaka 2007 pamoja na Sheria
ya Ardhi namba 4 ya 1999.
“(Sumaye) alitakiwa kutumia
shamba hilo kwa ajili ya kilimo tu na siyo kwa shughuli nyingine za ufugaji,
hilo ni kosa kwa mujibu wa sheria hizo. Kwa hiyo mchakato umeashaanza wa
kuligawa shamba hilo kwa wananchi na tunategemea miezi minne ijayo tutakuwa
tumemaliza taratibu zote,” alisema.
Desemba 15, 2015, Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alitangaza kiama kwa watu
wanaomiliki mashamba bila kuyaendeleza huku wakiyatumia kama dhamana ya kukopea
fedha benki.
Akizungumza kwa mara ya kwanza
baada ya kuteuliwa na Rais Magufuli, alisema kuna watu wamehodhi mashamba
makubwa lakini hawayaendelezi, hawayalipii kodi na mbaya zaidi, wanayatumia
kukopa fedha benki.
No comments