Wanaogushi Nyaraka Kuingiza Kemikali Wapigwa Marufuku.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele, akiongea na waandishi wa
habari kuhusiana na utaratibu unaohitajika
kufuatwa na wadau wa kemikali katika kuagiza kemikali kutoka Nje ya Nchi baada ya
kuonekana wadau wengi kutofuata kikamilifu taratibu husika. Wengine kutoka kulia
ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali, Bi. Josephine
Kalima, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara, Bw. George Kasinga na Kaimu
Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Ubora wa Bidhaa, Bw. Daniel Ndiyo.
Baadhi ya Watumishi wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na waandishi
wa habari wa kimsikiliza Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele
(hayupo pichani) wakati alipokuwa anazungumza na vyombo vya habari kuhusiana na
utaratibu unaohitajika kufuatwa na wadau wa kemikali katika kuagiza kemikali
kutoka Nje ya Nchi baada ya kuonekana wadau wengi kutofuata kikamilifu taratibu
husika. (Picha Ofisi ya Maabara ya Mkemia
Mkuu wa Serikali.)
Na Jacquiline Mrisho
na Bushiri Matenda - MAELEZO
Serikali imewapiga
marufuku mawakala wa forodha wanaogushi nyaraka kwa ajili ya kuingiza kemikali
kwani ni kinyume cha Sheria na pia wanaipotezea Serikali mapato.
Hayo yamesemwa leo
Jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Prof. Samwel Manyele
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uingizaji wa kemikali
nchini kutoka nje ya nchi.
Prof. Manyele amesema
kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali nchini kila
anayeingiza kemikali anatakiwa awe amesajiliwa na kupewa hati ya usajili huo
vile vile anatakiwa kupata idhini ya wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa
Serikali kabla ya kuagiza mzigo wa kemikali nchini.
“Natoa onyo kwa
mawakala wote wa forodha wasiofuata taratibu zilizowekwa na Serikali hasa
wanaogushi nyaraka zenye lengo la kukwepesha Sheria na kukwepa kulipa kodi na
tozo mbalimbali za Serikali hivyo watakaokaidi hatua kali za kisheria
zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Prof. Manyele.
Prof. Manyele amesisitiza
kuwa kuanzia Leo Agosti 17, 2017 hakuna mtu atakayeruhusiwa kujishughulisha na
shughuli za kemikali bila kuwa na hati ya usajili wa shughuli anayoifanya pia
hakuna atakayeruhusiwa kuagiza mizigo ya kemikali bila kuwa na kibali.
Aidha, Prof. Manyele
alifafanua lugha elekezi zinazotakiwa kutumika katika kuweka lebo za kemikali
husika kuwa ni Kiswahili na Kingereza tu hivyo hakuna kemikali itakayoruhusiwa
kuingia nchini ikiwa imendikwa kwa lugha tofauti na hizo.
Vile vile hakuna mdau
atakayeruhusiwa kushiriki tenda za ununuzi kwa ajili ya kuuza kemikali bila
kuwa na usajili kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
Ofisi ya Mkemia Mkuu
inaendelea kukabiliana na changamoto za wadau wa kemikali kwa kuendelea
kuwaelimisha wadau kuhusiana na matakwa ya Sheria na Kanuni za uingizaji wa
kemikali nchini, kuchukua hatua za kisheria kwa wale wanaokiuka matakwa ya Sheria
na kanuni zake, kuboresha mifumo, vifaa na sehemu za kufanyia kazi pia wakala
inaendelea kufanya kazi kwa masaa 24 katika siku saba za wiki.
No comments