Makamba: Serikali haina nia ya kurudisha viroba.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira), January Makamba amesema Serikali haina nia ya kurudisha sokoni
pombe zilizotengenezwa katika mifuko ya plastiki 'viroba' na kuwataka
Watanzania kupuuza uzushi unaoenezwa kwamba pombe hizo zitarudi.
Makamba alitoa kauli hiyo jana, Jumatatu Agosti 14 alipotembelea
eneo la Kimara Temboni lilipo ghala la kuhifadhi pombe mbalimbali ikiwamo
viroba linalomilikiwa na Kampuni Thema.
Makamba alisisitiza kwamba Serikali uamuzi wake wa
kuzuia pombe hizo upo palepale na haujabadilika hivyo watu waache kupotosha
wenzao.
"Baada ya kupiga marufuku kuna kampuni zilikuja
ofisini kuomba kuongezewa muda, lakini tuliwakatalia na kuwaambia waheshimu
uamuzi uliotolewa sasa hizi tetesi ya kwamba vinarudi sokoni sijui zinatoka
wapi," alisema Makamba.
Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli amesema njia
ya pekee kwa wafanyabiashara hao wa viroba wanaotakiwa kuifanya ili kupunguza
hasara ni kubadilisha pombe hizo na kuziweka katika chupa zenye ujazo
unaotakiwa.
Amesema kamwe Serikali haiwezi kurudi nyuma na kwamba
mafanikio yameanza kuonekana kutokana na hatua hiyo.
No comments