Wafuasi Wa Cuf Watimua Mbio Baada Ya Kuachiwa Huru Mahakamani Kukwepa Kukamatwa Tena Na Kufunguliwa Kesi Upya.
]Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewaachia huru wafuasi 22 wa
Chama cha CUF waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kukutwa na
mabomu ya machozi 10, ambayo yanatumiwa na Jeshi la Polisi.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mwambapa leo Jumanne, Agosti 15
amewaachia huru wafuasi hao chini ya kifungu cha 225 c ha mwenendo wa mashauri
ya Jinai (CPA).
Kesi hiyo ilikuwa katika hatua ya washtakiwa hao kusomewa maelezo
ya awali (PH) na leo washtakiwa hao walipaswa kusomewa, lakini Wakili wa
Serikali, Nassoro Katuga amedai kuwa walikuwa bado hawajayaandaa na akaomba
iahirishwe.
Hata hivyo, wakili wa washtakiwa hao, Hashimu Mziray hakuwa na
pingamizi lakini Hakimu Mwambapa kutokana na kesi hiyo kuahirishwa mara kwa
mara takribani mara sita aliifuta kesi hiyo na kuwaachia huru washtakiwa.
Baada ya washtakiwa hao kuachiwa huru askari polisi walianza
kuwakamata kitendo ambacho kilizua purukushani kwa sababu washtakiwa hao
walikuwa wakijikwamua mikononi mwa askari hao na kukimbia.
Hata hivyo, wengi wao walifanikiwa kukimbia na baadhi yao
walikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa askari hao.
Pia, washitakiwa hao wanaodaiwa kutenda makosa hayo kati ya
Zanzibar na Dar es Salaam wanatuhumiwa kuwa wanachama wa kikundi cha ‘Blue
Guard’, kinachojitwika mamlaka ya polisi.
Washitakiwa hao waliokuwa wakikabiliwa na kesi hiyo ni Hamis Omary
Hamis, Said Mohamed Zaharani, Hamid Nassoro au Hemed, Nassoro Humudi Ally,
Othuman Humud au Abdallah, Swalehe Ally Swalehe na Hamis Hamis Haj
Wengine ni Majid Juma, Mohamed Khamis Ally, Ramadhan Juma, Juma
Hamad Seif, Masoud Asa Fumu, Jecha Faki Juma, Mbaruku Bakari, Muhsin Ally Juma,
Juma Omary Hamis na Haji Rashid Juma.
Pia, wamo Ally Nassoro au Haji, Ally Juma Salum, Juma Haji au
Mmanga, Mohamed Amir Mohamed na Mohamed Zuberi.
Kwa pamoja walikuwa wakidaiwa kuwa Septemba 20 na 25, mwaka 2016,
katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar na Dar es Salaam na wenzao, ambao hawapo
mahakamani, walikula njama ya kutenda kosa kwa kuunda kikosi cha brigadi,
ambacho kinafanya kazi kama polisi kinyume cha sheria.
Washtakiwa hao pia wanadaiwa katika tarehe hizo na maeneo hayo,
wakiwa wanachama wa kikundi cha ‘Blue Guard’, kwa madhumuni ya kujiingiza
katika ajira, walikuwa wakifanya majukumu ya polisi.
Wanadaiwa kuwa Septemba 25, mwaka2016, maeneo ya Mwananyamala ‘A’,
wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, walikutwa wakimiliki visu vitano na mabomu
10 ya machozi.
Pia, wanadaiwa kuwa siku hiyo walikutwa wakimiliki mabomu hayo 10
ya machozi kinyume cha sheria, kwa kuwa kimsingi humilikiwa na Jeshi la
Polisi.Walikana mashtaka hayo na walikuwa wapo nje baada ya kukamilisha
masharti ya dhamana waliyopewa.
Washtakiwa hao wanatetewa na wakili Hashimu Mziray ambaye alilaani
kitendo cha askari hao wa polisi kuwakamata wateja wake bila ya kufuata utaratibu.
No comments