RUFAA VYETI FEKI: 600 WAGONGA MWAMBA, 450 WARUDISHWA KAZINI
Watumishi wa umma 450 walioondolewa
kazini kutokana na kudaiwa kutumia vyeti vya kughushi wamerudishwa kazini baada
ya kushinda rufaa zao.
Baada ya kutangazwa kwa Orodha ya
watumishi wenye vyeti feki, 1050 walikata Rufaa huku 8800 wakiridhika na
matokeo hayo.
Mbali na hilo, Serikali imesitisha
mishahara kwa watumishi wa umma ambao walitakiwa kuwasilisha vyeti vyao kwa
uhakiki lakini mpaka sasa hawajafanya hivyo.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Dk.Laurean Ndumbalo alisema watumishi hao wameshinda
rufaa zao hivyo wataandikiwa barua za kurudishwa katika utumishi wa umma.
Alisema katika rufaa hizo, wengi
walikuwa wanawake walioolewa na kubadili majina yao kwa kutumia ya waume zao.
“Kuna
baadhi walitumia majina mawili alipokuwa kidato cha nne baadaye alilazimika
kutumia matatu na kusababisha mkanganyiko hivyo tumejiridhisha na wanarudishwa
katika utumishi wa umma,” alisema Dk. Ndumbalo.
Alisema Serikali pia imesitisha
mishahara kwa watumishi wa umma ambao walitakiwa kuwasilisha vyeti vyao kwa
uhakiki lakini mpaka sasa hawajafanya hivyo.
“Serikali
imesitisha mishahara ya watumishi wote ambao muundo wa utumishi wao uliwataka
kuwa na sifa ya kufaulu kidato cha nne wakati wanaajiriwa lakini
hawakuwasilisha vyeti vyao kuhakikiwa na Baraza la Mitihani.
“Tunasitisha
mishahara yao kuanzia mwezi Julai hadi hapo watakapowasilisha vyeti vyao
kuhakikiwa,” alisema Dk. Ndumbalo.
Dk. Ndumbalo aliongeza kuwa kwa
watumishi walioajiriwa wakiwa darasa la saba kabla ya waraka wa Utumishi wa
Umma namba moja wa mwaka 2004 uliowataka waajiriwa kuwa na sifa ya kidato cha
nne, wataendelea na kazi mpaka watakapostaafu.
Alisema sera ya Menejimenti na Ajira
katika utumishi wa umma toleo la mwaka 1998 lilianza kutekelezwa Mei 20, 2004
hivyo kwa walioajiriwa kabla ya hapo warudishwe kazini kama waliondolewa kimakosa.
“Nasisitiza
kuwa watumishi wote wa umma walioajiriwa kwa sifa ya elimu ya darasa la saba
kabla ya Mei 20 hawahusiki na uhakiki wa vyeti vya kufaulu mtihani wa kidato
cha nne na wataendelea kuwa watumishi wa umma katika vyeo vyao mpaka watakapostaafu
kazi,” alisema Dk.Ndumbalo.
Aidha alisema serikali inatangaza
ajira mpya 10,184 katika sekta mbalimbali huku ikitoa ajira 3,172 kwa sekta ya
afya.
No comments