JAJI MUTUNGI: ATISHIA KUCHUKUA HATUA KALI ZA KISHERIA DHIDI YA CHADEMA NA CUF
Siku chache baada ya vyama vya
upinzani vya Chadema na CUF (Upande wa Profesa Ibrahim Lipumba) kutishiana
kuharibiana kupitia oparesheni zao mpya, msajili wa vyama vya siasa nchini,
Jaji Francis Mutungi amevionya vyama hivyo.
Chadema walikuwa wa kwanza kutangaza
kuingilia mgogoro ndani ya CUF wakitangaza kuanzisha ‘Oparesheni Ondoa Msaliti
Buguruni’ wakilenga kumuondoa mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na ofisi ya
Msajili, Profesa Ibrahim Lipumba.
CUF inayomuunga mkono Profesa Lipumba
pia ilijibu mapigo kwa kudai kuwa itakuja na ‘Oparesheni Futa Chadema’,
wakilaani kitendo cha Chadema kuingilia mgogoro huo.
Kufuatia kauli hizo, Jaji Mutungi
amevionya vyama hivyo kuwa vitakabiliwa na mkono wa sheria endapo vitajihusisha
na vurugu ya aina yoyote.
Msajili aliongeza kuwa ingawa
amesikia kupitia vyombo vya habari vitisho hivyo, hajapokea barua yoyote ya
malalamiko ofisini kwake kutoka kwa vyama hivyo.
“Natoa onyo kwa chama chochote cha
siasa ambacho kitaonesha ubabe na kutumia wafuasi wake waweze kufanya vurugu.
Tutakichukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria,” Jaji Mutungi anakaririwa na
Mtanzania.
“Kama kungekuwa na tatizo wangeleta
barua ofisini kwangu ya malalamiko, lakini mpaka sasa sijapata barua yoyote
inayohusiana na madai yao zaidi ya kusoma kwenye vyombo vya habari,” aliongeza.
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea
alifanya mkutano na vyombo vya habari hivi karibuni jijini Dar es Salaam na
kueleza kuwa wamebaini Profesa Lipumba anatumika kuidhoofisha CUF hali
itakayodhoofisha pia muungano wa Ukawa, hivyo wameamua kumuunga mkono Katibu
Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.
Kubenea alitangaza rasmi ‘Oparesheni
Ondoa Msaliti Buguruni’ akidai kuwa tayari ilishaanza wakiwa Bungeni mjini
Dodoma kwa kuwatenga wote wanaoshirikiana na Profesa Lipumba.
Saa chache baadae, Naibu Katibu Mkuu
CUF upande wa Bara, Magdalena Sakaya ambaye anatambuliwa na Ofisi ya Msajili na
anayemuunga mkono Profesa Lipumba alijibu mapigo kwa kueleza kuwa kambi yake
itakuja na ‘Oparesheni Futa Chadema’.
No comments