MBUNGE ASHUKIWA BUNGENI BAADA YA KUWATUHUMU WAPINZANI KULA HELA ZA RAMBIRAMBI ZA MSIBA WA NDESAMBURO
Mbunge wa viti maalumu (CCM), Jackline Ngonyani jana alizua
kizaazaa bungeni baada ya kuwaambia wabunge wa upinzani wamekosa dira kiasi cha
kula rambirambi zilizotolewa kwenye msiba wa Philemon Ndesamburo.
Alitoa kauli hiyo alipokuwa akichangia mjadala wa bajeti ya
mwaka 2017/18. Baada ya kuzungumzia hoja zake, Ngonyani alielezea kilichotokea
kwenye salamu za pole zilizotolewa wakati wa msiba wa muasisi huyo wa Chadema
aliyewahi pia kuwa mbunge wa Moshi Mjini kwa vipindi vitatu mfululizo.
Mbunge huyo alianza kwa kumpongeza Rais John Magufuli kwa
utekelezaji wa ilani ya CCM na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo
inawagusa wananchi, akidai utekelezaji huo unawanyima hoja wapinzani.
Aliyafananisha maneno ya wapinzani na miti kuteleza siku ya kifo
cha nyani, akisema licha ya kueleza kwamba Rais anatumia sera zao, wapinzani
hao wamesahau changamoto zinazowakabili wananchi kwenye majimbo yao.
Mbunge huyo alimshambulia mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche
na wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari.
Alimshangaa Heche kwa kuomba muongozo kutokana na wananchi wa
jimbo lake kuvamia mgodi wa North Mara ulio chini ya kampuni ya Acacia baada ya
kukabiliana na askari polisi.
Mwenyekiti wa kikao hicho, Mussa Azzan Zungu alimtaka
kuwasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba kupata ufafanuzi wa
suala hilo kutoka serikalini.
“Huyu Heche aliongea humu ndani kuhusu wananchi wake kulinda
mgodi, leo anajikosha kwa kuomba muongozo. Rais hakusema watu wakavamie migodi,
hao wakamatwe kama wahalifu wengine. Huyu naye akamatwe na kuunganishwa pamoja
na wavamizi hao,” alisema.
Baada ya kauli hiyo, Heche alisimama na kumpa taarifa mbunge
huyo kwa kueleza kwamba jina lake linatumika vibaya. Alikumbusha kwamba
wananchi wake walifuatilia uwasilishaji wa ripoti ya kamati na kufahamu kwamba
kampuni hiyo ni feki.
“Nilisema sisi tumeumizwa, sasa kama unafikiri naogopa
kuunganishwa hebu njoo unikamate wewe,” alisema.
Baada ya taarifa hiyo, Jackline alimwambia Heche: “Usinipotezee
muda, nina mambo mengi ya kuzungumza.”
Baada ya kuachana na Heche, mbunge huyo alimvaa Nasari kwa
kueleza kwamba alitumia dakika 10 alizopewa kulalamika juu ya uharibifu
uliofanywa kwenye shamba la maua la mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
“Hizi ni akili au matope? Wananchi wake hawana changamoto? Ni
mambo ya aibu sana,” alisema mbunge huyo akikaribia kuhitimisha mchango wake
kwenye mjadala huo.
Kabla hajakaa, sauti ilisikika ikimkumbusha suala la kuliwa kwa
fedha za msiba huo, kengele ya kuisha kwa muda wake ikiwa imeshagongwa, alitupa
kijembe wa upinzani.
“Nakushukuru sana mwenyekiti, naunga mkono hoja na (wapinzani)
waache kula rambirambi za msiba wa Ndesamburo,” alisema Ngonyani.
Kauli hiyo iliwafanya wabunge wa upinzani wacharuke na kumtaka
afute maneno hayo.
Alikuwa ni mbunge wa viti maalumu (Chadema), Cecilia Pareso
aliyemng’ang’ania baada ya kutoa taarifa kwamba kilichozungumzwa na Jackline si
sahihi na kumtaka kufuta maneno hayo au kuthibitisha tuhuma hizo.
Mbunge huyo alikubali kuyaondoa maneno yake kwenye kumbukumbu
kutokana na kukosa ushahidi wa alichokisema.
“Mwenyekiti, kwa sababu ni suala la msiba, nayaondoa maneno
hayo,” alisema na kuhitimisha suala hilo lililowagusa wabunge wengi wa upinzani
waliokuwapo kwenye kikao cha jana asubuhi.
No comments