LHRC KUPINGA KUONGEZWA MUDA WA LESENI YA UZALISHAJI UMEME KWA KAMPUNI YA IPTL
TAMKO
KWA VYOMBO VYA HABARI
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni shirika lisilo la kiserikali
lenye maono makuu ya kuona Jamii yenye Haki na Usawa Tanzania. Kituo cha Sheria
na Haki za Binadamu kimejikita katika utetezi wa Haki za Binadamu ikijumuisha
haki za maendeleo.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa mshangao
na masikitiko makubwa kinapingana na hatua ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na
Maji (EWURA) kupokea na kutangaza kupitia gazeti la serikali la Daily News, la
siku ya Jumatano Juni 7, 2017 kusudio la kuiongezea leseni ya uzalishaji umeme
kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), kampuni ambayo
inahusishwa na kashfa nzito ya uchotwaji wa mabilioni kupitia akaunti ya
ESCROW.
Ikumbukwe kwamba Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) mwaka
2014 ilitoa mapendekezo mbali mbali juu ya umiliki wa mitambo ya IPTL ikiwemo,
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uchunguzi juu ya
umiliki na uwepo wa rushwa katika utendaji kazi wa IPTL na wabia wake.
Mapendekezo ambayo mpaka sasa
hayajafanyiwa kazi huku umma wa watanzania ukiachwa katika bumbuwazi.
Mbali na kutokuwepo kwa taarifa sahihi juu ya
upotevu mkubwa wa fedha za watanzania katika sakata la ESCROW, tumeshangazwa na
kitendo cha EWURA kutaka maoni ya wadau huku ikiwa inafahamu fika kuwa mikataba
kati ya Serikali na IPTL ni ya siri na hivyo wadau hawana sababu za kimkataba
za kutoa mapingamizi au maoni.
Kutokana na sintofahamu hii, Chombo hiki chenye
mamlaka ya udhibiti wa Nishati na Madini kilipaswa kujiridhisha juu ya
mapendekezo ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Kamati ya
Hesabu za Serikali juu ya utata wa umiliki wa IPTL na kashfa za rushwa
zinazoizunguka badala ya kutaka maoni au mapingamizi kutoka kwa wananchi na
wadau ambao hawajui undani wa mkataba wa IPTL na Serikali.
Kwa kuzingatia misingi ya uwajibikaji wa Serikali
na makampuni, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa mapendekezo
yafuatayo:
1. EWURA kusitisha mara moja kusudio hili la
kukusanya maoni ya kuiongezea muda kampuni ya IPTL mpaka serikali
itakapotekeleza mapendekezo yote ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kupitia kamati yake ya mwaka 2014.
2. EWURA kujiridhisha uhalali wa kisheria juu ya
umiliki, kujiridhisha pasipo shaka ushiriki wa IPTL katika suala zima akaunti
ya ESCROW na tuhuma za rushwa kwa wamiliki wake.
3. EWURA kuomba radhi watanzania na wabunge kwa
kujaribu kuirudisha IPTL kwa jamii huku ikitambua wazi miaka 3 iliyopita IPTL
ilikuwa kwenye kashfa nzito iliyozua mtafaruku ndani na nje ya Tanzania.
4. LHRC, inaikumbusha jamii nzima ya watanzania,
waheshimiwa wabunge, viongozi wa dini na vyama vya siasa kuungana pamoja kwa
ajili ya maslahi ya umma katika kukata kusudio hili la kuongezewa leseni ya
kuzalisha umeme nchini wakati kampuni tajwa imetiliwa shaka ya kuwa na dosari
nyingi.
5. Serikali kutoa majibu na ufafanuzi wa
utekelezwaji wa maazimio ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania juu ya
kampuni ya IPTL.
6. Serikali kupitia taasisi zake kuacha kufanya
mazingaombwe kwa wananchi kwa kuwashirikisha katika shughuli ambazo hawajui
misingi yake na badala yake wawe wazi katika hatua zote za makubaliano na
wawekezaji.
Mwisho; Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
kinaamini vyombo vya habari vitakuwa mstari wa mbele kukumbusha namna Bunge na
wadau wengine walivyosimama kidedea kuipinga kampuni ya IPTL baada ya kuibuka
kwa sakata la ESCROW.
Imetolewa
Alhamisi Juni 8, 2017
Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji
No comments